1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wasifu wa Denis Mukwege

Zainab Aziz
20 Desemba 2023

Mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel, Denis Mukwege mwenye umri wa miaka 68 ni miongoni mwa wagombea wa urais nchini Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo katika uchaguzi wa Desemba 20.2023.

https://p.dw.com/p/4aPeY
Kandidaten für die Präsidentenwahl in der Demokratischen Republik Kongo Denis Mukwege
Picha: Nils Petter Nilsson/TT/picture alliance

Denis Mukwege mwenye umri wa miaka 68 alizaliwa tarehe mosi, Machi mwaka 1955 katika Kongo ya Ubelgiji ambayo leo hii ndiyo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Ni mtoto wa tatu kati ya watoto tisa wa mchungaji wa kanisa la Pentekoste na mkewe. Mukwege karibu afe wakati wa kuzaliwa kwake kutokana na kupata maambukizi, lakini maisha yake yaliokolewa na mmisionari wa kanisa la Pentekoste, mkunga raia wa Sweden, bibi Majken Bergman.

Elimu

Denis Mukwege alisomea nchini mwake Kongo na kisha akasomea udaktari katika nchi jirani ya Burundi. Alipokuwa mtoto Mukwege aliongozana na baba yake mchungaji kuwatembelea wagonjwa katika mji wa Bukavu ulioko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Walikwenda kumwona mvulana mmoja aliyekuwa mgonjwa sana. Yeye na baba yake walimwombea kijana huyo, lakini Mukwege hakuweza kufanya zaidi ya hilo na wakati huo alikuwa na miaka minane. Lakini siku hiyo ndipo alipoamua kwamba angetaka kuwa daktari pindi atakapokuwa mkubwa. Alimwambia baba yake kuwa ''wewe baba unaweza kutuongoza kati kusali, lakini mimi nataka kuwaponya watu kwa kuwa daktari na hivyo kuwaponesha wagonjwa kwa kuwapa dawa."

Baada ya masomo yake nchini Burundi, alirejea nyumbani Kongo na kufanya kazi katika hospitali ya Lemera ya mashariki mwa jimbo la Kivu Kusini, ambako alikumbana na wanawake waliokabiliwa na madhila kutokana na kuathiriwa sehemu zao za siri. Hali hiyo ilimfanya Mukwege aondoke na kwenda nchini Ufaransa ambako alikwenda kubobea katika mafunzo yaliyojikita kwenye magonjwa ya wanawake na masuala ya uzazi.

Daktari Bingwa

Leo hii Denis Mukwege ni daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake duniani. Kutokana na kiwango kikubwa cha unyanyasaji wa kijinsia katika eneo la vita ambavyo vimetikisa mashariki mwa Kongo kwa zaidi ya miongo miwili, amebobea katika matibabu ya wanawake wanaobakwa wakati wa vita.

Mnamo mwaka 2018, Denis Mukwege alitunukiwa Tuzo ya Amani ya Nobel kwa pamoja na mwanaharakati wa jamii ya WaYazidi, Nadia Murad kutokana na juhudi za kukomesha unyanyasaji wa kijinsia na pia kutumiwa unyanyasaji huo kama silaha ya vita.  Vilevile amepokea tuzo nyingine nyingi kwa huduma zake bora anazotoa kwa walionusurika na ubakaji.

Mnamo mwaka 1999 alianzisha hospitali ya Panzi, inayotoa huduma bora kabisa ambapo waathiriwa wapatao elfu 50 wametibiwa kwenye hospitali hiyo iliyo nje ya mji wa Bukavu.

Mshindi huyo wa Tuzo ya Amani, Denis Mukwege, kweli anaweza kuwa ni mgeni kwenye uwanja wa siasa, lakini kwa muda mrefu amekuwa mkosoaji mkubwa wa serikali. 

Baada ya miezi kadhaa ya uvumi, hatimaye Denis Mukwege alitangaza rasmi nia yake ya kuwania urais mapema mwezi Oktoba 2023.

Katika kampeni za kuwania urais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ameahidi kuzingatia haki, utu na uaminifu. Pia ameahidi kuumaliza umaskini, migogoro na ufisadi nchini Kongo iwapo atashinda kwenye uchaguzi huu wa leo.

Mtazamo wa umma

Taswira ya umma ya Mukwege ni safi, lakini haieleweki vyema katika nchi kubwa ya Kongo. Hana idadi kubwa ya wapiga kura na hakuwa na ufadhili wa kutosha wa fedha ambazo zingemuwezesha kuendesha kampeni kwa ufanisi.

Chanzo: AFP