1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wasifu wa Seif Sharif Hamad

3 Novemba 2010

Mwalimu wa skuli na mtaalamu huyu wa sayansi ya siasa ni mmoja wa wanasiasa waandamizi wa zama za baada ya Mapinduzi ya 1964 anayewania urais wa Zanzibar kwa mara ya tano sasa.

https://p.dw.com/p/PwKj
Mwenyekiti na mgombea urais wa chama cha CUF, Seif Shariff HamadPicha: DW

Hamad, ambaye anajulikana zaidi Visiwani na Bara kama Maalim Seif amekuwa akisiisitiza siku zote kwamba alishinda chaguzi zote tatu ziliopita, lakini Tume ya Uchaguzi Zanzibar ilikataa kuheshimu uamuzi wa wananchi na kuamua kuyaghushi matokeo ili kuwapa ushindi wapinzani wake.

Maaalim aliweka wazi kuwa ijapokuwa zilikuwepo dosari katika uchaguzi wa Jumapili alikubali matokeo na kumpongeza Dk. Shein kw ushindi kwa maslahi ya Zanzibar na watu wake ili kuepusha mfarakano.

Maalim Seif ambaye alisherehekea siku yake ya kuzaliwa ya kutimia miaka 67 katika mkutano wa kampeni na kulishwa keki na mke wake, Bi Awena Sinani, wiki mbili ziliopita, anaangaliwa na watu wengi kama ni mtu ambaye ni muwazi sana na kwa ujasiri anasisitiza umuhimu wa kutambuliwa kama nchi na kutaka iwachiwe kutumia rasilmali zake inavyoona ni kwa maslahi ya Wazanzibari bila ya kuingiliwa na Bara ambayo iliungana nayo mwaka 1964 kuunda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Msimamo wake usiotetereka wa kutaka pawepo na uwazi kuonyesha mambo mambo gani ya Muungano na masuala gani ni yale ambayo Zanzibar ina mamlaka kamili ya kujiamualia yamempatia marafiki na maadui.

Baadhi ya watu waliopo Bara wana wasi wasi kwamba Maalim Seif ambaye alifukuzwa kutoka chama tawala cha CCM mwaka 1987 na moja kwa moja kupoteza wadhifa wake wa Waziri Kiongozi wa serikali ya Mapinduzi Zanzibar anataka kuudhoofisha Muungano. Lakini kwa Wazanzibari wengi na hasa katika kisiwa cha Pemba ambako anatoka anaonekana ni mzalendo mwenye uchungu na Zanzibar.

Alizaliwa kutokana na familia ya wakulima wa kijiji cha Mtambwe, nje kidogo ya mji wa Wete, Pemba, katika mwaka 1943, Maalim Seif alivuka bahari ya mkondo wa Pemba kuja Zanzibar kuendelea na masomo ya sekondari kutoka 1958 hadi 1963.

Hakuweza kuendelea na masomo ya chuo kikuu pale alipotakiwa aende kusomesha katika shule za sekondari ili kujaza mapengo yaliowachwa na walimu wengi wa Kiingereza na wachache wa kizalendo baada ya Mapinduzi ya 1964. Wakati ule siasa kali za utawala wa mkono wa chuma ulishuhudia serikali ikitaifisha vikataa vidogo vya mashamba na nyumba za makazi za watu walioonekana maadui wa Mapinduzi ziliipelekea Zanzibar kuelezwa na nchi za Magharibi kama Cuba ya Afrika Mashariki.

Hata hivyo, alifanikiwa kuchukua shahada ya kwanza ya Elimu, Sayansi ya Kisiasa na Uhusiano wa Kimataifa´kutoka mwaka 1972 hadi 1975 na aliporudi Zanzibar alichaguliwa msaidizi maalum wa Rais wa Zanzibar mpaka mwaka 1977 alipochaguliwa Waziri wa Elimu.

Katika medani ya siasa Maalim Seif alichaguliwa mjumbe wa Halamshauri Kuu ya Taifa ya CCM ambayo aliitumikia kwa miaka 11. Katika mwaka 1984 kufuatia kile kilichojulikana kama kuchafuka kwa hali ya hewa ya kisiasa Visiwani kulikoshuhudia kulazimishwa kustaafu kwa aliyekuwa Rais wa pili wa Zanzibar, Sheikh Aboud Jumbe, Maalim Seif alichaguliwa Waziri Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Lakini kauli zake za uwazi za mara kwa mara za kuonyesha hafurahishwi na mwenendo mzima wa Muungano na kueleza Zanzibar haitendewi haki kwa baadhi ya mambo ndani ya Mungano kuliepelea kutimuliwa katika chama na pia kupoteza wadhifa wa Waziri Kiongozi kufuatia hatuahio ya chama.

Tokea wakati huo aliandamwa kwa kuonekana tishio la kisiasa na mwaka 1989 alifunguliwa mashitaka bandia ya kupatikana na nyaraka za siri za serikali. Alikaa miaka miwili gerezani, baadhi ya wakati katika chumba akiwa peke yake kwa muda unaoweza kufikia wiki mbili mpaka alipoachiwa na Mahakama ya Rufaa ya Tanzania kwa kuwa hakuwa na kesi ya kujibu.

Tanzania ilipofungua milango yake na kuruhusu mfumo wa vyama vingi vya siasa mwaka 1992, Maalim Seif na baadhi ya wenzake aliofukuzwa nao Halmashauri Kuu ya CCM walikuwa miongoni ma walioanzisha Chama chaWananchi (CUF) na kuwa Makamo Mwenyekiti wake wa kwanza na sasa Katibu Mkuu.

Aligombea Urais wa Zanzibar katika uchaguzi wa kwanza wa mfumo wa vyama vingi mwaka 1995, mwaka 2000 na 2005. Alishindwa kwa kura chache, lakini mwenyewe amekuwa akiamini alishinda chaguzi zote hizo na aliporwa ushindi kwa sababu Tanzania na hasa Zanzibar haijakuwa tayari kupokea mfumo wa demokrasia kwa moyo safi.

Mandhari iliopo baada ya uchaguzi wa Jumapili ni tofauti na iliokuwepo katika chaguzi tatu ziliopita ambapo mshindi alichukua kila kitu.

Katika uchaguzi wa safari hii mshindi anatakiwa aunde serikali ya umoja wa kitaifa. Nini kitatokea baada ya Dk Shein kutangazwa mshindi kitatoa mwanga kama Zanzibar itaendelea na hali ya kisiasa ya watu wake kuelewana na kuvumiliana au itarudi katika zama za siasa za chuki na uhasama ambazo zilionekana kuigawa Zanzibar katika mapande mawili, moja linalokiunga mkono chama tawala cha CCM na jengine chama cha upinzani cha CUF.

Mwandishi: Salim Said Salim
Mhariri: Oummilkheir Hamidou