1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wasiwasi kuhusu kudunguliwa ndege ya Uturuki

Josephat Nyiro Charo24 Juni 2012

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon ameelezea wasiwasi wake mkubwa kuhusu athari za kudunguliwa kwa ndege ya kivita ya Uturuki na Syria.

https://p.dw.com/p/15KTz
A Turkish Air Force F-4 war plane fires during a military exercise in Izmir, in this May 26, 2010 file photo. Turkey lost a F-4 warplane, similar to the one pictured, over the Mediterranean on June 22, 2012, but Turkish Prime Minister Tayyip Erdogan said in his first public comments, he could not say whether the plane had crashed or been shot down. REUTERS/ Osman Orsal/Files (TURKEY - Tags: MILITARY CIVIL UNREST TRANSPORT POLITICS)
Ndege ya kivita ya UturukiPicha: REUTERS

Kwenye mazungumzo yake kwa njia ya simu na waziri wa mashauri ya kigeni wa Uturuki, Ahmet Davutoglu, katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, alisema hatua ya Syria kuidunguliwa kwa ndege ya Uturuki inaweza kuzua athari kubwa katika eneo zima.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa, Martin Nesirky, amesema Ban Ki Moon ameipongeza Uturuki kwa kujizuia kuchukua hatua ya haraka kulipiza kisasi. Amezishukuru Uturuki na Syria kwa kufanya operesheni ya pamoja kuitafuta ndege hiyo pamoja na marubani wake. Ban Ki Moon amezhimiza nchi hizo mbili kuendelea kulishughulikia suala hilo kidiplomasia na kuahidi msaada wa Umoja wa Mataifa katika hali hiyo ngumu.

U.N. Secretary-General Ban Ki-moon, addresses the audience at the 'Sustainable Energy for All' Summit in Brussels, Monday, April 16, 2012. (Foto:Yves Logghe/AP/dapd)
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki MoonPicha: dapd

Uturuki imethibitisha kuwa ndege yake aina ya F-4 Phantom huenda iliingia anga ya Syria bila kibali kabla kudunguliwa Ijumaa iliyopita (22.06.2012), katika kauli inayoonekana kutuliza hali ya wasiwasi kati ya mahasimu hao wa zamani.

Kudunguliwa kwa ndege hiyo kumeongeza hali ya wasiwasi kati ya mataifa hayo ambayo yamekuwa washirika wakubwa, kabla kuanza maandamano ya mapinduzi nchini Syria yaliyodumu miezi 15. Tukio hilo linaashiria kuwa mapinduzi hayo yanaenea nje ya mipaka ya Syria. Ujerumani na Irak ni miongoni mwa nchi zilizotoa mwito kuwepo na hali ya kujizuia katika eneo hilo.

Operesheni ya kuwatafuta marubani

Waziri wa mambo ya kigeni wa Uturuki, Ahmet Davutoglu, alikutana jana na maafisa wa jeshi kutathmini hatua za kuchukua na kuratibu operesheni ya kuwatafuta na kuwaokoa marubani wa ndege hiyo ambao hawajulikani waliko. Waziri mkuu wa nchi hiyo, Recep Tayyip Erdogan, anatarajiwa kukutana na viongozi wa vyama vya upinzani leo kujadili tukio hilo. Uturuki inachunguza njia iliyosafiria ndege hiyo pamoja na data zake kuthibitisha kama ilikuwa ikiruka katika anga ya Syria wakati ilipodunguliwa.

U.N. Secretary-General Ban Ki-moon, addresses the audience at the 'Sustainable Energy for All' Summit in Brussels, Monday, April 16, 2012. (Foto:Yves Logghe/AP/dapd)
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki MoonPicha: dapd

Hapo jana Syria ilisema iliidungua ndege ya Uturuki kwa sababu iliingia katika anga yake na kusisitiza kwamba halikuwa shambulizi. Uturuki imetishia kulipiza kisasi lakini haikusema ni hatua gani itakayochukua huku ikiendelea kuwatafuta marubani wa ndege hiyo ambao hawajulikani waliko.

Uturuki imesema ndege hiyo ilianguka katika bahari ya Mediterania, kiasi kilometa 13 kutoka mji wa Latakia nchini Syria. Syria imedai ndege hiyo ilikiuka sheria na kuingia katika anga yake upande wa baharini bila kibali, kwa umbali wa kilometa kama moja. Ilisema vikosi vya Syria vilitambua ilikuwa ndege ya Uturuki baada ya kuishambulia.

Mwandishi: Josephat Charo/APE/AFPE

Mhariri: Bruce Amani