1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

120311 Japan Reaktor

13 Machi 2011

Hatma ya kinu cha nyuklia cha Fukushima Daichi, na vinu nyengine vya nyuklia katika pwani ya mashariki ya Japan vinabakia katika hali ya kutia wasiwasi kufuatia tetemeko la ardhi

https://p.dw.com/p/10YIs
Maafisa wa polisi waliovaa vichuja hewa wapiga doria nje ya kinu cha FukushimaPicha: AP

Shirika la kimataifa la kuzuia kuenea kwa silaha za nyuklia, IAEA, linasema wahandisi katika kinu cha nyuklia kilichoharibiwa kaskazini mwa mji mkuu wa Japan Tokyo wameanza kutumia maji ya baharini yaliyochangwa na kemikali aina ya boron kusaidia kupunguza uharibifu uliosababishwa na mlipuko mkubwa. Mlipuko huo ulitokea kufuatia tetemeko kubwa la ardhi nchini humo Ijumaa iliyopita, lililokuwa la ukubwa wa 8.9 katika kipimo cha Richter.

Hatma ya kinu cha nyuklia cha Fukushima Daichi, yapata kilomita 240 kaskazini mwa Tokyo na vinu nyengine vya nyuklia katika pwani ya mashariki ya Japan vinabakia katika hali ya kutia wasiwasi kufuatia tetemeko hilo. Shirika la Japan linaloshughulikia masuala ya nyuklia na usalama wa viwanda, NISA, limsema wahandisi wamekuwa waking'anga'ana kupunguza shinikizo katika vinu hivyo ili kuzuia kuyeyuka kwa mitambo katika vinu hivyo.

Juhudi za serikali

Kufuatia kuvuja kwa miale ya nyuklia aina ya caesium 137 na iodine 131 katika eneo lililo karibu na kinu cha nyuklia cha Fukushima, shirika la NISA limesema kwene tovuti yake kwamba viwango vya miale hiyo angani vimeonekana vikipungua. Msemaji wa serikali ya Japan, Yukio Edano amesema wanafanya mambo mawili kwa wakati mmoja: kutoa hewa nje ya kinu hicho na wakati huo huo kutia maji.

Msemaji huyo aidha amesema miale ya nyuklia iliyovuja sio mingi vile kiasi cha kuathiri afya ya wananchi. Edano amesema kulighulikia janga la tetemeko la ardhi litahitaji jitihada kubwa za kitaifa kwa kuwa ni janga lisilo na mithili. Kutahitajika pia ushirikiano mkubwa kati ya vikosi vya usalama na mashirika mengine. "Lengo letu ni kuokoa maisha na tunatarajia kiasi cha dola bilioni 2.4 katika bajeti ya mwaka huu kutosha, lakini ni vigumu kukadiria fedha zitakazohitajika katika bajeti ya mwaka ujao wa kibiashara unaoza Aprili mosi. Bunge litakuwa na jukumu la kuamua." amesema afisa huyo.

Premierminister Japan Naoto Kan zum Erdbeben
Waziri mkuu wa Japan Naoto KanPicha: AP

Vyombo vya habari vya Japan vimemkosoa waziri mkuu wa nchi hiyo, Naoto Kan, kwa jinsi serikali yake inavyoushulikia mlipuko uliotokea katika kinu cha nyuklia cha Fukushima, uliozusha hofu ya kuvuja kwa miale ya nyuklia angani. Naoto Kan amesema ameamuru watu umbali wa kilomita 20 kutoka kinu hiyo waondoke.

Kitisho cha Chernobyl

Wakati huo huo, wataalamu wa nyuklia wa Marekani wameonya juu ya kutokea mkasa kama ule wa Chernobyl nchini Ukraine uliotokea mnamo mwaka 1986 na ule mwingine katika kinu cha nyuklia cha kisiwa cha Three Mile katika jimbo la Pennsylvania nchini Marekani mnamo mwaka 1979. Robert Alvarez, anayeshughulikia masuala ya kupunguza silaha za nyuklia katika taasisi ya mafunzo ya sera, amesema hali imekuwa ya kukatisha tamaa mno kiasi kwamba Wajapani hawana uwezo wa kupata maji safi au maji yasiyo na chumvi kupoza mitambo katika kinu chake cha nyuklia cha Fukushima, na sasa wamelazimika kugeukia maji ya baharini.

Polisi ya Japan umesema leo kwamba idadi ya vifo vilivyosababishwa na tetemeko la ardhi inakaribia 900, huku watu 642 wakiwa hawajulikani waliko. Watu 1,570 walijeruhiwa katika tetemeko hilo la Ijumaa iliyopita.

Mwandishi: Josephat Charo

Mhariri: Mohamed Khelef