1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wasyria waitisha maandamano mengine makubwa

16 Machi 2012

Wanaharakati Syria wametoa wito wa kufanyika maandamano nchi nzima kudai "vikosi vya kimataifa viingilie kati haraka" huku mjumbe maalum wa kimataifa, Kofi Annan, akijiandaa kuzungumza na Baraza la Usalama.

https://p.dw.com/p/14LXg
Maandamano dhidi ya Rais Bashar al-Assad nchini Syria.
Maandamano dhidi ya Rais Bashar al-Assad nchini Syria.Picha: AP

Kupitia ukurasa wa Facebook walioupa jina la "Mapinduzi ya Syria 211" , wanaharakati wanaopigania mageuzi wamewataka wananchi waandamane kote nchini humo, kama wanavyofanya kila siku ya Ijumaa, lakini safari hii kauli mbiu ikiwa "kudai watumwe haraka wanajeshi kutoka nchi za Kiarabu, Kiislam na za nyengine zilizosalia za dunia".

Wanadai pia pawepo eneo la lisiloruhusiwa kuruka ndege na la nchi kavu ili kufungua njia ya kuingizwa misaada ya kiutu.

Upande wa upinzani unazidi kupaza sauti kudai nchi za kigeni ziingilie kati haraka, huku mataifa kadhaa ya Kiarabu, na hasa katika Ghuba yamekuwa kila wakati yakisema yanaunga mkono wapinzani wapatiwe silaha.

Mataifa sita ya Kiarabu katika Ghuba ya Uajemi yameamua kufunga ofisi zao za ubalozi mjini Damascus. Katibu Mkuu wa Baraza la Ushirikiano la Nchi za Ghuba, Abdelatif al-Zayani, amesema uamuzi huo umepitishwa ili kulalamika dhidi ya ukandamizaji wa serikali ya Bashar al-Assad inayoendelea kuwauwa raia, na kupinga juhudi zote zilizolengwa kuupatia ufumbuzi mzozo uliopo. "Kabla ya hapo Saud Arabia na Bahrein zilitangaza kufunga ofisi zao za ubalozi mjini Damascus.

Raia 45 wanasemekana wameuliwa katika mkoa wa Idlib, karibu na mpaka na Uturuki, habari hizo zimetangazwa na shirika la haki za binaadamu la Syria lenye makao yake makuu mjini London.

Rais Bashar al-Assad na mke wake, Asma.
Rais Bashar al-Assad na mke wake, Asma.Picha: picture-alliance/dpa

Kabla ya hapo shirika hilo lilizungumzia juu ya maití 23 zilizogunduliwa andani ya shimo moja karibu na Idlib. Baadhi ya maiti hizo zilikuwa zimefungwa pingu mikononi na kufungwa vitambaa machoni. Kwa mujibu wa shirika hilo, maiti zote zinaonyesha wahanga waliuliwa kwa kupigwa risasi.

Nchini Syria kwenyewe maelfu ya watu waliteremka majiani jana kumuunga mkono Rais al-Assad na serikali yake. Licha ya miito ya kumaliza mzozo, Rais Bashar al Assad anasema kwamba watashinda njama dhidi yake.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergei Lavrov, amesema Urusi inatumia maingiliano yake na serikali ya Syria kuitanabahisha ishirikiane kikamilifu na mjumbe wa kimataifa, Kofi Annan.

Leo mchana, Katibu Mkuu huyo wa zamani wa Umoja wa Mataifa anapanga kuliarifu Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa njia ya mkutano wa video kutoka Geneva, matokeo ya juhudi zake za kuumaliza mzozo wa Syria.

Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/AFP/Reuters
Mhariri: Miraji Othman