1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wataalamu wa uchunguzi wafika katika eneo la ajali

1 Agosti 2014

Maafisa nchini Ukraine wamesema leo(01.08.2014) kuwa kiasi wanajeshi 10 wa jeshi la serikali wameuwawa katika mapigano na wapiganaji wanaotaka kujitenga, wanaoiunga mkono Urusi upande wa mashariki mwa nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/1CnLd
Ukraine MH17-Absturz Wrackteil vom Flugzeug
Mabaki ya ndege ya shirika la ndege la MalaysiaPicha: Reuters

Nao wachunguzi wa kimataifa wanakwenda katika eneo hilo la ajali kwa mara ya pili leo.

Maafisa wa jeshi wamesema katika taarifa kuwa shambulio la kushitukiza dhidi ya majeshi ya serikali lilitokea wakati vikosi vya jeshi hilo vikipelekwa katika mji wa Shakhtarsk, mji ambao umekuwa eneo la mapigano makali kwa siku kadhaa. Taarifa hiyo haikufafanua lini shambulio hilo lilitokea.

Ukraine Arseny Yatseniuk Premierminister Kiev
Waziri mkuu wa Ukraine Arseny YatseniukPicha: Reuters

Bunge lapitisha sheria muhimu

Wakati huo huo, jana bunge la Ukraine lilikataa ombi la kujiuzulu kwa Waziri Mkuu Arseny Yatseniuk na hatimaye limepitisha sheria ambayo Waziri Mkuu huyo alisema ilikuwa inahitajika kuweza kugharamia mashambulizi ya jeshi la nchi hiyo dhidi ya wapiganaji wanaotaka kujitenga upande wa mashariki mwa Ukraine, na kuepusha nchi hiyo kushindwa kulipa madeni yake.

Kukubali kwa bunge hilo kupitisha sheria ambazo ilikataa kuzipitisha wiki moja, kabla kunatoa ahueni kwa mataifa ya Magharibi yanayoiunga mkono Ukraine, ambayo yalikuwa yakihofia kuwa Ukraine inatumbukia katika mvurugiko mkubwa wa kisiasa na huenda ikashindwa kupata fedha za uokozi kutoka jumuiya ya kimataifa wakati ikielekea katika kipindi cha uchaguzi.

Mapambano ya kisiasa yamekuwa yakiendelea huku kampeni ya kijeshi ikiendelea kuyakamata tena maeneo ya jimbo la Donbass, ambalo linapakana na Urusi kutoka kwa wapiganaji wanaoiunga mkono Urusi.

Ostukraine Angriffe 1.8.2014
Mapambano mashariki mwa UkrainePicha: picture-alliance/dpa

Wataalamu wa kimataifa wanajaribu tena leo Ijumaa kuanza uchunguzi ambao umekwama katika eneo la ajali ya ndege ya shirika la ndege la Malaysia wakati huo huo majeshi ya Ukraine yakitishia kuanza tena kwa mashambulizi dhidi ya wapiganaji wanaoiunga mkono Urusi baada ya siku moja ya kusitisha mapigano.

Uchunguzi waendelea katika eneo la ajali

Uchunguzi wa kimataifa mashariki mwa Ukraine uliendelea jana wakati wataalamu walipojiweka katika hatari ya kushambuliwa na hatimaye kufika katika eneo la ajali kwa mara ya kwanza baada ya uchelewesho wa karibu wiki moja baada ya Ukraine kutangaza kusitisha mashambulizi yake.

MH17 Flugzeugabsturz Absturzstelle Ukraine 18.7.2014
Wachunguzi wa shirika la OSCE katika eneo la ajaliPicha: imago/Itar-Tass

Mwakilishi wa Shirika la Usalama na uUhirikiano barani Ulaya, OSCE, Alexander Hug amesema kuwa wamefanikiwa kufika salama mahali hapo:

"Tumeweza kufika katika eneo hilo leo bila tukio lolote. Tulicheleweshwa njiani lakini hatimaye tuliwasili mchana, tukabaki hapo hadi saa tisa mchana na kisha tukarejea kwa njia hiyo hiyo tuliokuja nayo bila tukio lolote, na kutoka katika eneo la wapiganaji na kuingia katika eneo linalodhibitiwa na serikali, na muda mfupi kabla mji wa Donetsk kurejea mikononi mwa waasi."

Kikosi kidogo cha wataalamu kutoka Uholanzi na Australia kikiwa pamoja na waangalizi wa kimataifa waliingia katika eneo hilo baada ya mapigano makali kati ya majeshi ya serikali na wapiganaji kusitishwa. Polisi wa Uholanzi ambao wanaongoza uchunguzi wa kimataifa wamesema hali kuzunguka eneo hilo ilipoangukia ndege hiyo bado ni ya hatari licha ya kikosi hicho kidogo cha wataalamu kuweza kufika katika eneo hilo.

Alexander Hug Deputy Chief Monitor OSCE Ukraine
Mwakilishi wa OSCE Alexander HugPicha: OSCE/Jonathan Perfect

Jeshi la Ukraine limetangaza hapo kabla siku moja ya kusitisha mapigano katika eneo lote la mashariki baada ya wito kutoka kwa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, wa kusitisha mapigano kuzunguka eneo la ajali, ambako miili ya wahanga 298 bado iko juani wiki mbili baada ya ndege hiyo kudunguliwa kwa kombora katika eneo linaloshikiliwa na waasi.

Mwandishi: Sekione Kitojo/afpe/rtre/ape

Mhariri: Mohammed Khelef