1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wafungwa wanne wa ugaidi wahamishiwa Oman, moja Estonia

Admin.WagnerD15 Januari 2015

Wizara ya ulinzi ya Marekani Pentagon, imesema kwamba wafungwa watano katika gereza la Marekani la Guantanamo wamepelekwa katika nchi nyengine. Wanne kati ya hao wamepelekwa Oman na mwengine nchini Estonia.

https://p.dw.com/p/1EKmO
Symbolbild - Guantanamo
Picha: Getty Images/J. Moore

Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya Wizara ya ulinzi ya Marekani, wafungwa wanne waliopelekwa katika falme ya Ghuba ya Oman ni Al Khadr Abdullah, Muhammad al-Yafi, Fadel Hussein Saleh Hentif, Abd Al-Rahman Abdullah Au Shabati na Mohammed Ahmed Salam. Mwenzao wa tano amepelekwa nchini Estonia.

Kiasi ya watu 122 bado wangali katika gereza hilo la Guantanamo , linalotumiwa kuwaweka watu wanaoshukiwa kuhusika na ugaidi, kufuatia mashambulizi ya Septemba 11 mwaka 2001 mjini New York na wengi wao hawajashtakiwa.

Wizara ya ulinzi ya Marekani imezishukuru Oman na Estonia kwa kuonyesha ishara hiyo iliotajwa kuwa ni ya kiutu pamoja na moyo wa kuiunga mkono Marekani katika juhudi za kulifunga gereza hilo la Guantanamo.

Gereza la Guantanamo.
Gereza la Guantanamo.Picha: AFP/Getty Images/M. Antonov

Republicans wataka kuzuwia kuachiwa kwa wafungwa

Hatua hiyo ya kuwahamishia wafungwa hao watano katika nchi hizo mbili, imekuja siku moja tu baada ya wajumbe kadhaa wa chama cha Republican katika Baraza la Seneti akiwemo Kelly Ayotte kutoka New Hampshire kutaka paweko na sheria ya kuzuwia kuachiwa kwao wakisema bado ni hatari kwa Marekani na washirika wake.

Rais Barack Obama ameahidi kulifunga gereza hilo ,linalolaaniwa kimataifa na ambalo lilifunguliwa mwaka 2002, katika kampeni ya Marekani dhidi ya ugaidi. Juhudi zake zimekwamishwa na wabunge akiwemo Seneta John McCain anayeupinga mpango huo.

McCain, Mrepublican aliyekuwa mpinzani wa Obama katika Uchaguzi wa Rais mwaka 2008 alisema wiki iliopita kwamba, asilimia 30 ya wafungwa walioachiwa kutoka katika gereza hilo wamerejea katika mapambano dhidi ya Marekani.

Msimamo wa Obama

Lakini hivi karibuni Rais Obama aliahidi kuharakisha juhudi za kulifunga gereza la Guantanamo na utawala wake ukawahamisha wafungwa 28 mwaka jana.

Wafungwa wa Guantanamo huwekwa chini ya ulinzi mkali.
Wafungwa wa Guantanamo huwekwa chini ya ulinzi mkali.Picha: picture-alliance/dpa/M. Shephard

Mjumbe wa Rais huyo aliyehusika na zoezi la kuachiwa huru wafungwa hao Cliff Sloan alijiuzulu mwezi Desemba baada ya kuripotiwa kwamba amevunjika moyo na jinsi wizara ya ulinzi inavyochelewa kuidhinishwa kuachiwa wafungwa na kupelekwa nchi nyengine .

Miongoni mwa wafungwa 122 waliobakia baada ya watano kupelekwa Oman na Estonia jana, imethibitishwa kuwa 44 wakiwemo raia wa Yemen wameonekana wanaweza kupelekwa nchi nyengine, wakati waliobakia wanatajwa kuwa ni hatari kuachiwa huru.

Mashirika ya haki za binaadamu yamelitaja gereza la Guantanamo kuwa " Shimo jeusi," ambalo wafungwa husota kwa miaka mingi bila ya kufikishwa mahakamani.

Mwandishi: Mohamed Abdul-Rahman ,AFP DPA,REUTERS
Mhariri: Daniel Gakuba