1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watano wauawa Yemen, 15 nchini Syria

Mohammed Khelef3 Desemba 2011

Hata baada ya kusainiwa kwa makubaliano ya Rais Ali Saleh kuondoka madarakani nchini Yemen, na jitihada ya Jumuiya ya Kiarabu kumaliza machafuko ya Syria, bado mauaji yamekuwa yakiendelea katika mataifa hayo.

https://p.dw.com/p/13Lxl
Mama akilia mbele ya picha ya mwanawe aliyeuawa nchini Syria.
Mama akilia mbele ya picha ya mwanawe aliyeuawa nchini Syria.Picha: picture alliance / dpa

Raia watatu na wapiganaji wawili wanaoipinga serikali wameuawa kufuatia mashambulizi ya vikosi vya serikali ya Yemen katika mji wa Taiz. Kwa mujibu wa taarifa za kitabibu, raia waliouawa ni wa familia moja na waliuawa kwenye nyumba yao huku wapiganaji wawili wakiuawa kwenye mapambano, dhidi ya vikosi vinavyomtii Rais Ali Abdullah Saleh. Maiti zote tano zimepelekwa kwenye hospitali ya Al-Rawda katikati ya mji wa Taiz ambao uko mikononi mwa waandamanaji wanaompinga Saleh.

Wakati huo huo, mapigano kati ya wanajeshi walioasi, na vikosi vya serikali ya Syria yamesababisha vifo vya watu 15 hivi leo. Kwa mujibu wa Shirika la Haki za Binaadamu la Syria, lenye makao makuu yake nchini Uingereza, mapigano yaliyotokea alfajiri katika mji wa Idilo, yamesababisha wanajeshi saba na askari polisi mmoja, wanajeshi watano walioasi na raia watatu.

Shirika la Haki za Binaadamu la Umoja wa Mataifa limesema wiki hii kuwa sasa Syria ipo katika ukingo wa kutumbukia kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe, na kwamba zaidi ya watu 4,000, wameshauawa tangu katikati ya mwezi Machi, mwaka huu.

Hadi katika siku za karibuni, umwagaji damu mkubwa ulikuwa ukifanywa na vikosi vya serikali tu baada ya kuwafyatulia risasi waandamanaji, lakini sasa kumekuwa na taarifa za wanajeshi walioasi na raia wenye silaha kupambana na vikosi vya serikali.