1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ni uchaguzi wenye ushindani mkubwa

24 Oktoba 2015

Wananchi wa Tanzania moja ya nchi kutoka katika mataifa ya Afrika ya mashariki, jumapili hii wanapiga kura kuchagua Rais na wabunge katika uchaguzi mkuu wa nchi humo.

https://p.dw.com/p/1GthN
Bendera ya Tanzania
Bendera ya TanzaniaPicha: Imago

Pande mbili zenye ushindani mkubwa katika uchaguzi huo za chama tawala CCM, na chama cha Demokrasia na maendeleo Chadema ambacho mgombea wake anaungwa mkono na umoja wa katiba ya wananchi nchini humo ( UKAWA ) zote jumamosi hii zimefunga kampeni zao kwa vishindo vya aina yake, wakati CCM, wakikamilisha kampeni zao huko katika uwanja wa CCM kirumba Mwanza , kwa upande wao wale wa UKAWA, wamekamilisha kampeni zao katika viwanja vya Jangawani jijini Daresalaam.

Ni dhahiri kuwa kutakua na mabadiliko katika uongozi wa taifa hilo kwani Rais wa sasa anayemaliza muda wake Jakaya Mrisho Kikwete hatagombeatena nafasi hiyo baada ya kuwa ametumikia tayari vipindi vyake viwili vya uongozi.

Wagombea ambao wanapewa nafasi kubwa ya kushinda katika nafasi hiyo ya Urais ni wa chama cha mapinduzi CCM, John Pombe Magufuli na mgombea wa chama cha Demokrasia na maendeleo CHADEMA kinachoungwa mkono na vyama vinavyounda umoja wa katiba ya wananchi UKAWA, Edward Ngoyai Lowasa.

Magufuli ambaye katika baraza la mawaziri linalomaliza muda wake alikuwa waziri wa ujenzi kiasi cha kupachikwa jina la "Tinga Tinga" kutokana na ufanisi wake katika wizara hiyo, awali hakuonekana kupewa nafasi kubwa kushinda kuwania nafasi hiyo kupitia chama chake caha mapinduzi ( CCM ) lakini hata hivyo baadaye alifanikiwa kupitishwa na wajumbe wa chama chake na kuibuka mshindi kati ya wanachama wengine 38 waliokuwa wamejitokeza.

Magufuli ambaye anatokea kaskazini magharibi mwa Tanzania katika wilaya ya Chato, pembezoni mwa ziwa Victoria alitunukiwa shahada ya udaktari wa falsafa katika somo la Kemia ya chuo kikuu cha Daresalaam miaka kadhaa iliyopita. Ni mbunge tangu 1995.

.

Ama kwa upande wake mgombea anayepeperusha bendera ya CHADEMA; ikiungwa mkono na UKAWA, Edward Lowasa, alijiunga na chama hicho akitokea chama cha mapinduzi CCM mwishoni mwa mwaka huu kutokana na kile alichosema ni mizengwe aliyofanyiwa na ukandamizaji wa demokrasia ndani ya chama hicho cha mapinduzi.

Lowasa ambaye ana shahada ya pili katika masuala ya maendeleo aliyoisomea huko nchini Uingereza, amewahi kushika nyadhifa mbalimbali katika serikali ya nchi hiyo, ikiwa ni pamoja na kuwa waziri katika wizara kadhaa, kabla ya kuteuliwa kuwa waziri mkuu wa nchi hiyo hadi alipojiuzuru nafasi hiyo wakati wa sakata la Richmond nchini humo miaka karibu minane iliyopita.

Lowasa aongeza hamasa katika kambi ya upinzania

Tangu kuingia upinzani akijiunga na chama cha CHADEMA Lowassa ambaye baadaye alifuatiwa na waziri mkuu mwingine wa zamani , Fredrick Sumaye kujitoa CCM ameonekana kuongeza hamasa ndani ya muungano huo wa UKAWA, hali inayofanya uchaguzi huo wa kesho kuwa na ushindani mkubwa. Pigo kubwa jengine kwa chama tawala lilikuwa n i kujitoa kwa mmoja wa waasisi wa chama hicho na mtu aliyesimamia falsafa ya chama, kingunge Ngombale Mwiru ambaye alisema kujitoa kwake miongoni mwa sababu nyengine , ni chama hicho kukosa dira na kukiuka katiba yake .

Wakati watanzania wakijiandaa kuamua Jumapili juu ya mustakbali wa taifa lao kwa miaka mitano ijayo, kinachozungumzwa na wengi ni amani na matarajio ya kuheshimiwa uamuzi wa wapiga kura . Katika hilo macho yanaelekezwa kwa Tume ya taifa ya Uchaguzi NEC.

Mwandishi: Isaac Gamba

Mhariri : Mohammed Abdul-Rahman