1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watanzania wamkumbuka Nyerere wakielekea uchaguzi mkuu

George Njogopa14 Oktoba 2015

Nchini Tanzania leo ni kumbukumbu ya kifo cha Baba wa Taifa hilo, Hayati Mwalimu Julius Nyerere, huku mada kuu inayotawala ikiwa ni uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika hapo Oktoba 25.

https://p.dw.com/p/1GnsR
Mwalimu Julius K. Nyerere (1922 - 1999)
Mwalimu Julius K. Nyerere (1922 - 1999)Picha: Getty Images/AFP

Kumbukukumbu hiyo inafanyika wakati ambapo chama tawala, Chama cha Mapinduzi (CCM) alichokiasisi Mwalimu Nyerere kikiwa katika mtihani mkubwa baada ya kuondokewa na vigogo kadhaa waliohamia upinzani.

Miaka 16 ni mingi lakini hekaya na nukuu za kiongozi huyo zinatawala siasa za Tanzania hasa wakati huu wa kuelekea kwenye uchaguzi mkuu, uchaguzi ambao hakuna mwanasiasa anayeweza kubashiri matokeo yake kutokana na ushindani mkubwa unaojitokeza.

Mwalimu Nyerere anatizamwama kama ramani halisi ya nchi ya Tanzania kutokana na misingi aliyoingejea Tanzania iliyozingatia umoja na mshikamano na huku pia akikemea vikali siasa zinazopalilia misingi ya kidini na ukabila.

Maadhimisho hayo yanafanyika huku pilika pilika za uchaguzi mkuu zikiwa zimepamba moto huku chama tawala CCM kikiendelea kupata pigo kutokana na baadhi ya vigogo wake kuendelea kukitupa mkono.

Nafasi ya Nyerere kwenye uchaguzi


Ukiweka kando mwanasiasa wa siku nyingi wa chama hicho, Kingunge Ngombale, Mwiru ambaye sasa amekuwa akuzunguka katika majukuwaa ya upinzani, baada ya kukikacha chama chake, hapo jana ramani ya siasa ilisomeka vingine baada ya mwanadiplomasia mkongwe, Juma Mwapachu, naye kutangaza kuachana na chama hicho.

Ingawa baadhi ya wachambuzi wa mambo wanaona kuwa Mwapachu, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, hakuwa katika majukwaa hai ya CCM, lakini kuondoka kwake kuna ishara inayozungumza kuhusu hatima ya chama hicho.

Ama katika hatua nyingine, baadhi ya makundi ya watu wamekuwa wakihoji mwenendo wa siasa zinazojitokeza sasa katika majukwaa kutokana na baadhi ya wanasiasa hao kutizingatia utashi halisi aliouasisi Mwalimu Nyerere na badala yake wamekuwa wakijitumbukiza katika siasa za chuki, udini na ukabila. Pamoja na kusifia ukuaji wa demokrasia, wengi wanawataka wanasiasa hao kuzingatia hoja zitakazolinufaisha taifa.

Uchaguzi wa mwaka huu unatarajiwa kuwa na mvutano wa aina yake kutokana na mambo kadhaa likiwamo hili na vigogo wa chama tawala kwenda upinzani.

Mwandishi: George Njogopa
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

Mgombea urais wa Tanzania kupitia upinzani, Edward Lowassa (kushoto) na wa CCM, John Magufuli.
Mgombea urais wa Tanzania kupitia upinzani, Edward Lowassa (kushoto) na wa CCM, John Magufuli.Picha: picture-alliance/AP Photo/Getty Images/AFP/DW Montage