1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watetezi wa haki wataka uchunguzi Kenya

John Juma4 Julai 2016

Makundi ya kutetea haki za kibinadamu ya kitaifa na kimataifa yanataka uchunguzi kufanywa kuhusu mauaji ya kiholela yanayodaiwa kufanywa na vyombo vya usalama dhidi ya raia. Hii ni baada ya kuuawa kwa wakili.

https://p.dw.com/p/1JIeB
Maandamano dhidi ya mauaji ya kiholela Nairobi.AC
Watetezi wa haki wataka uchunguzi kufanywa KenyaPicha: DW/A. Kiti

Maafisa nchini Kenya lazima wachunguze kwa dharura mauaji ya watu watatu wiki jana, akiwemo wakili wa kutetea haki za kibinadamu, na wale watakaopatikana na hatia wachukuliwe hatua mahakamani. Hayo yamesemwa na mashirika 34 ya kitaifa na kimataifa yanayotetea haki za kibinadamu.

Wito huu unajiri huku wanaharakati wa kutetea haki za kibinadamu wakifanya maandamano jijini Nairobi na miji mingine ya Kenya kuyalaani mauaji hayo ya kikatili.

Wakili Willie Kimani, mteja wake na dereva wake walitekwa nyara, wakatoweshwa na baadaye kupatikana wameuawa na miili yao kutupwa katika mto, kilomita 73 kaskazini mashariki ya Nairobi. Watetezi wa haki za kibinadamu wanasema hali hiyo inaibua hofu kuhusu hali ya haki za kibinadamu na uzingatifu wa sheria nchini Kenya, hasa ikizingatiwa kuwa ripoti zinaonyesha maafisa wa polisi walihusika.

Haya mauaji ya kiholela ni ukumbusho wa kuwa haki ya kutafuta haki ya kibinadaamu inakiukwa na inevunjwa. Amesema Muthoni Wanyeki ambaye ni mkurugenzi wa shirika la kutetea haki za kibinadamu Amnesty International katika maeneo ya Afrika Mashariki, Pembe ya Afrika na Maziwa makuu.

Ameongeza kuwa afisi huru inayochunguza matendo ya polisi IPOA, lazima ianzishe uchunguzi wa kipekee na huru kwa haraka kuhusu, utekaji nyara, kutoweshwa na kuuawa kwa watatu hao, kwa dhamira ya kuwafungulia washukiwa mashtaka.

Polisi wakikabiliana na waandamanaji.
Polisi wakikabiliana na waandamanaji.Picha: Reuters/G. Tomasevic

Mwili wa wakili Willie Kimani, ambaye alikuwa mwajiriwa wa shirika la kutetea haki za kibinadaamu na misaada International Justice Mission lenye makao yake makuu nchini Marekani, pamoja na miili ya dereva wake na wa mteja wake Josephat Mwenda ilipatikana katika mto Ol-Donyo Sabuk katika kaunti ya Machakos, mashariki ya Kenya tarehe 30 mwezi Juni. Hiyo ikiwa ni wiki tatu baada ya watatu hao kutoweka kwa njia ya kutatanisha.

Polisi washukiwa kuhusika

Ripoti za awali zilidokeza kuwa afisa mmoja wa polisi wa utawala, ambaye alimshtaki Menda huenda ndiye aliwateka nyara. Watatu hao walionekana mara ya mwisho wakitoka katika mahakama ya Mavoko kaunti ya Machakos tarehe 23 Juni 2016 baada ya kusikizwa kwa kesi yao.

Maafisa wa polisi wa utawala katika kituo cha Syokimau walimfungulia Mwendwa kesi mnamo Disemba 2015, miezi kadhaa baada ya yeye kuwasilisha malalamiko katika shirika huru la IPOA dhidi ya afisa mmoja mkuu wa polisi ambaye alimpiga risasi bila hatia pale alipokuwa akishuka kwenye pikipiki yake aliposimamishwa na maafisa wa polisi.

Makundi ya kutetea haki za kibinadamu yamesema yanao ushahidi kuwa watatu hao walizuiliwa katika kituo cha polisi wa utawala Syokimau muda mfupi kabla ya ripoti za kutekwa nyara kwao kuibuka. Tangu hapo taarifa za wapi walikuwa zilisalia kutojulikana hadi miili yao ilipopatikana siku saba baadaye.

"Kwamba mauaji haya yanajiri baada ya misururu ya madai sawa na hayo katika maeneo mengine ya nchi kuchunguzwa, yanaibua swali tete la ikiwa maafisa nchini Kenya wapo tayari kukomesha mauaji ya kiholela," amesema Henry Maina ambaye ni mkurugenzi wa shirika la Article 19 katika Afrika Mashariki. Amesisitiza kuwa rais Kenyatta laazima achukue hatua madhubuti kuhakikishia wakenya na jamii ya kimataifa kuwa serikali inachukuliwa kwa uzito suala la mauaji ya kiholela yanayofanywa na polisi.

Polisi akimpiga mwandamanaji.
Polisi akimpiga mwandamanaji.Picha: picture alliance/AP Photo/B. Curtis

Polisi wazuiliwa rumande

Polisi watatu wanaodaiwa kuhusika katika mauaji hayo walikamatwa na kufikishwa mahakamani mapema leo. Hakimu mkuu Aniel Ogembo ameamuru washukiwa hao Frederick Leliman, Stephen Chebulet na Sylvia Wanjiku kuzuiliwa kwenye rumande kwa siku 14 ili kuruhusu uchunguzi kamili kukamilishwa.

Katika muda huo, miili ya marehemu pia itafanyiwa uchunguzi kubaini aina ya mapigo au dhuluma waliyotendewa kabla ya kufa au kutupwa mtoni. Mkurugenzi wa tume ya kitaifa ya kutetea haki za kibinadamu Kenya George Kegoro amesema mauaji hayo ya kikatili yanapaswa kuwa wito kwa rais Kenyatta kubuni tume maalum kufanya uchunguzi dhidi ya polisi kama asasi inayotumia visivyo nguvu na mamlaka yake, kwa manufaa ya kibinafsi au kuendeleza uhalifu.

Mataifa washirika wa Kenya hasa Sweden, Uingereza na Marekani yanayofadhili polisi ya Kenya yametakiwa kushinikiza maafisa wa Kenya kuhakikisha uchunguzi kamili umefanywa. Kufadhili vyombo vya usalama vya Kenya bila kuhakikisha vinawajibika kulinda haki za kibinadamu hufanya mataifa yanayofadhili pia kuchangia katika ukiukaji wa haki za kibinadamu.

Nao mawakili nchini humo wametangaza mgomo wa wiki nzima. Wametsema hawatafika katika mahakama kuwakilisha wateja wao, kama njia moja ya kukemea mauaji ya mwenzao na mauaji ya kiholela kwa jumla yanayoendelea nchini Kenya.

Mwandishi: John Juma

Mhariri: Iddi Ssessanga