1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watoto wa umri mdogo katika migodi ya madini katika jamhuri ya kidemokrasia ya Congo

Gregoire Nijimbere16 Oktoba 2006

Maelfu ya watoto wanaharatisha maisha yao kwa kufanya kazi katika migodi ya madini katika mkoa wa Katanga kusini mashariki mwa jamhuri ya kidemokrasia ya Congo. Shirika la Umoja wa mataifa linalowahudumia watoto, UNICEF na mashirika mengine yasiokuwa ya kiserikali, yamekuwa yakijaribu kuwaokoa watoto hao.

https://p.dw.com/p/CHmN
Mtoto akibeba mzigo wa madini ya Kobalti katika mgodi wa Shinkolobwe karibu na mji wa Likasi, DRC
Mtoto akibeba mzigo wa madini ya Kobalti katika mgodi wa Shinkolobwe karibu na mji wa Likasi, DRCPicha: AP

Eneo la Katanga ni lenye asili mali nyingi za madini ya Shaba, Kobalti na Koltani. Kazi ya kuchimba madini hayo yalipewa kampuni ya kiserikali ya madini, Gecamines, ambayo kwa sasa imeanza kuporomoka.

Mwaka wa 1986, kampuni hiyo ya Gecamines, ilizarisha tani laki 5 za shaba. Lakini tangu karibuni mwaka wa 2003, uzarishaji ulipungua hadi kufikia tani15,000 tu.

Kufirisika kwa kampuni hiyo ya Gecamines kulisababisha hasara kubwa pia katika mashirika yaliokuwa na ushirikiano na kampuni hiyo ambayo ilikuwa hata ikigharimia ujenzi wa miundo mbinu hama shule na hospitali. Sekta zote hizo ziliathiriwa kutokana na kuanguka kwa Gecamines, alisema Raf Costermans, muakilishi wa shirika la kujitegemea, Group One, katika mkoa wa Katanga.

Kwa sasa, shughuli za uchimbaji madini katika migodi mkoani huko Katanga, huendeshwa na watu wa kawaida kukiwemo watoto wenye umri mdogo kuweza kuanza kazi na hasa kazi ngumu kama hiyo ya kuchimba madini.

Kulingana na mashirika yasiokuwa ya kiserikali, NGO’s, wengi wa watoto hao hupatikana katika migodi ya sehemu za Kolowezi, kusini na vile vile sehemu za Likasi na Lubumbashi. Shirika la Group One linasema miongoni mwa watu 140,000 wanaoshiriki katika shughuli za uchimbaji madini katika mkoa wa Katanga, kati ya 50,000 na 100,000 ni watoto chini ya umri wa miaka 18.

Raf Costermans wa shirika la Group One, alisema asili mia 65 ya watoto hao katika sehemu za Lubumbashi aidha waliacha shule au wanagawa muda kati ya shule na migodi. Mara nyingi, alizidi kusema Costermans, watoto hao ndiwo wanaowahudumia wadogo zao na ikiwa ni yatima, matumaini ya kurejea shuleni ni madogo mno.

Katika shughuli hizo za madini, watoto hubeba mizigo mizito na kuvuta pumzi zenye hewa ya chuma au madini mengine.

Madhara yake ni magonjwa yanayojitokeza kama ugonjwa wa macho hata kansa.

Watoto hao hutumika bila tahadhari yoyote na ajali zimekuwa nyingi. Hutumia maji machafu na wakati mwingine hutumia alkohol au mihadharati kuwaongezea nguvu.

Kulingana na shirika hilo la Group One, katika kijiji cha Shinkolobwe, karibu na mji wa Likasi, kuna ghala ya mabaki ya madini ya uranium ambayo inasemekana yalitoa uranium iliotumiwa kutengeneza bomu la kinyuklia lililotumiwa na Marekani katika vita vikuu vya pili vya dunia.

Watoto katika sehemu hiyo huzaliwa na ulemavu mkubwa, baadhi yao huzaliwa bila akili.

Katika maeneo ya madini, wasichana wanakwenda huko kufanya kazi ya ukahaba na kuongeza kasi ya kutapakaa virusi vya ukimwi.

Kwa ushirikiano na shirika la Umoja wa mataifa linalowahudumia watoto UNICEF, mashirika yasiokuwa ya kiserikali yameanza kutoa huduma kwa watoto hao na kuwahamasisha viongozi na raia kuhusu athari zinazowakabili watoto wanaoshiriki katika shughuli za migodi.

Kundi la kwanza la watoto 250 chini ya umri wa miaka 15, walirejeshwa katika maisha ya kawaida na sasa wanasoma. Kundi la pili la idadi kama hiyo, wanatarajiwa kurudishwa shuleni mwezi ujao. Mpango wa chakula duniani WFP, huwasaidia kwa chakula cha mchana. Mashirika hayo yasiokuwa ya kiserikali, yameanza pia kuwasaidia wazazi katika miradi ya kimaendeleo ili wawe na pato na hivyo kuwaepusha watoto wao kujiunga na kazi hizo hatari za madini.