1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu 13 wauawa katika shambulizi la gari mjini Barcelona

Isaac Gamba
18 Agosti 2017

Kiasi ya watu 13 wameuawa huku wengine 100 wakijeruhiwa baada ya gari  kuendeshwa katika umati mkubwa wa watu kwenye mtaa ambao ni maarufu kwa kutembelewa na watalii mjini Barcelona Uhispania.

https://p.dw.com/p/2iRGq
Spanien | Lieferwagen fährt in Barcelona  in eine Menschenmenge | Polizei und Forensiker untersuchen den Tatort
Picha: REUTERS/Stringer

 Polisi nchini humo wamethibitisha tukio hilo kuwa ni shambulizi lakigaidi. Dereva wa gari hilo ametoweka na bado anaendelea kusakwa. Tayari watu wawili wanaoshukiwa kuhusika na tukio hilo wametiwa mbaroni  huku mtu mmoja akiuawa baada ya kuendesha gari kupita kizuizi cha polisi kwa ajili ya ukaguzi. 

Afisa mmoja wa taasisi inayohusika na ulinzi wa raia nchini humo amesema miongoni mwa waliojeruhiwa katika tukio hilo ni raia wa mataifa ya kigeni kutoka Ufaransa, Ujerumani , Ubelgiji, Uholanzi, Australia, Argentina na Italia.

Bendera kupepea nusu mlingoti

Spanien Madrid - Premierminister Mariano Rajoy bei Pressekonferenz
Waziri Mkuu wa Uhispania Mariano RajoyPicha: Getty Images/AFP/P.-P. Marcou

Waziri Mkuu wa Uhispania Mariano Rajoy ametangaza siku tatu za maombolezo ambapo bendera nchini humo zitapepea nusu mlingoti.Wakati huohuo Kansela wa ujerumani Angela Merkel ametuma salaamu za rambirambi kwa serikali ya Uhispania kufuatia tukio hilo linalodaiwa kuwa ni shambulizi la kigaidi. Msemaji wa Kansela Merkel Steffen Seibert ameandika katika ukurasa wa twitter kuwa Kansela Merkel amesema anaungana na wananchi wa Uhispania katika kipindi hiki kigumu. Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May naye pia amelaani shambulizi hilo.

 

Mwandishi: Isaac Gamba/afpe

Mhariri     :Iddi  Sessanga