1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu 15 wauwawa kwenye mapigano ya kikabila Kenya

25 Januari 2008
https://p.dw.com/p/CxlT

Mapigano ya kikabilia yamewaua watu wasiopungua 15 hii leo katika mkoa wa bonde la ufa nchini Kenya na kuwalazimu maelfu ya watu wengine kuyakimbia makazi yao.

Kuzuka kwa machafuko mapya nchini humo kunavuruga matumaini ya kumalizika kwa ghasia ambazo zimekuwa zikiendelea nchini Kenya kwa majuma kadhaa kufuatia kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi wa mwezi Disemba mwaka jana.

Shirika la msalaba mwekundu nchini humo limesema mji wa Nakuru umefungwa na wafanyakazi wake mjini humo wamepeleka maiti tatu na mamia ya majeruhi katika hospitali moja ya mjini humo.

Jana katibu mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa, Kofi Annan, alifaulu kuwakutanisha Raila Odinga na rais Kibaki kwa mara ya kwanza tangu mzozo wa kisiasa ulipoanza. Odinga ameahidi kufanya kila jitihada kuhakikisha amani inarejea nchini Kenya.

Hii leo kiongozi wa upinzani Raila Odinga amefutilia mbali uwezekano wa kuchukua wadhifa wa waziri mkuu katika serikali itakayoongozwa na rais Mwai Kibaki.

Kiongozi huyo pia ameutaka Umoja wa Afrika usimtambue Kibaki kama rais wa jamhuri ya Kenya wakati utakapokutana katika makao yake makuu mjini Addis Ababa nchini Ethiopia kuanzia tarehe 31 mwezi huu hadi tarehe 2 mwezi ujao.

Bwana Odinga ameutaka umoja huo usimruhusu Kibaki apeleke ujumbe wake katika mkutano huo.