1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu kadhaa wajeruhiwa shambulizi la basi Jerusalem

19 Aprili 2016

Watu 21 walijeruhiwa katika mlipuko wa bomu ndani ya basi mjini Jerusalem hapo jana (18.04.2016) katika kile ambacho polisi imekieleza kuwa ni shambulizi la kigaidi.

https://p.dw.com/p/1IYJ4
Jerusalem Bus Bombe Explosion
Picha: Reuters/R.Zvulun

Shambulizi hilo linaibua hofu ya kuanza tena mfululizo wa mashambulizi ya mabomu yanayofanywa na watu wa kujitoa muhanga yaliyoshuhudiwa katika miji mikubwa ya Israel muongo mmoja uliopita.

"Bila shaka hili lilikuwa shambulizi la kigaidi," alisema kamishna wa polisi wa mji wa Jerusalem, Yoram Halevy, na kuongeza kuwa ni mapema kumtambua mshambuliaji au kusema ikiwa ni shambulizi la bomu lililofanywa na mtu wa kujitoa muhanga.

Basi lengine na gari dogo lililokuwa karibu liliharibiwa na mlipuko huo. Msemaji wa polisi ya Israel, Micky Rosenfeld, alithibitisha watu 21 walijeruhiwa katika hujuma hiyo, wawili vibaya sana.

"Polisi ya Israel inaendelea na uchunguzi kuhusiana na mlipuko ndani ya basi mjini Jerusalem kubaini kama ni shambulizi la kigaidi ama la. Kuna watu wawili tunaotaka kuwahoji ambao bado wangali hospitali wakitibiwa. Usalama umeimarishwa kote Jerusalem na polisi wanapiga doria katika maeneo mbalimbali kuepusha na kukabiliana na matukio yoyote ya mashambulizi ya kigaidi."

Awali polisi walisema wanachunguza uwezekano kwamba tatizo la kiufundi lilisabisha moto ulioyaunguza mabasi hayo mawili katika barabara ya Derech Hebron, katika eneo la kusini magharibi la Jerusalem karibu na mpaka na eneo linalokaliwa na Israel la Ukingo wa Magharibi.

Israel Jerusalem Bus Explosion Wrack
Maafisa wa usalama na waokoaji wakikusanyika kando ya basi lilishambuliwaPicha: Getty Images/AFP/T. Coex

Kundi la Hamas linaloutawala Ukanda wa Gaza limetao taarifa likipongeza shambulizi la bomu dhidi ya basi lakini halikusema lilihusika. Baadhi ya misikiti ya Gaza pia imepongeza shambulizi hilo kutumia ujumbe uliotangazwa kupitia vipaza sauti. Msemaji wa Hamas nchini Qatar, Husam Badran, alisema, "Shambulizi hili linathibitisha kwa kila mtu kwamba watu wetu hawataacha njia ya upinzani."

Netanyahu aapa kulipiza kisasi

Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, ameapa kulipiza kisasi. "Mjini Jerusalem mabasi mawili yameshambuliwa katika shambulizi la kigaidi. Nawatakia afueni ya haraka wote waliojeruhiwa. Tutawatafuta waliofanya shambulizi hili. Tutawafikia waliowatuma na wale wote wanaowaunga mkono. Tuko katika vita dhidi ya ugaidi - ugaidi wa kutumia visu, mashambulizi ya risasi, mabomu na ugaidi katika mahandaki."

Netanyahu anatarajiwa kwenda Moscow Alhamisi wiki hii kukutana na rais wa Urusi, Vladimir Putin, kujadili njia za kuafikia makubaliano ya amani kati ya Israel na Wapalestina. Rais Putin alimuambia rais wa mamlaka ya ndani ya Wapalestina jana kwamba anaunga mkono juhudi za kutafuta amani Mashariki ya Kati.

"Ninaweza kukuhakikishia kwamba tutaunga mkono juhudi zote unazofanya kuweka mazingira yanayohitajika kuufungulia mlango mdahalo wa maana," alisema Putin wakati alipozungumza na Abbas katika ikulu ya Kremlin.

Golanhöhen israelischer Ministerpräsident Benjamin Netanjahu
Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin NetanyahuPicha: Getty Images/AFP/S. Scheiner

Katika kipindi cha miezi sita iliyopita, mashambulizi ya barabarani ya Palestina yamewaua Waisraeli 28 na raia wawili wa Marekani waliokuwa wakiitembelea Israel. Vikosi vya Israel vimewaua Wapalestina wasiopungua 191, huku Israel ikisema 130 walikuwa washambuliaji. Wengine wengi walipigwa risasi na kuuliwa wakati wa makabiliano na maandamano.

Muisraeli atiwa hatiani kwa mauaji ya Mpalestina

Wakati huo huo, mahakama ya Israel leo imemtia hatiani mwanamume wa Israel kwa utekaji nyara na mauaji ya kijana wa Kipalestina mwaka 2014, baada ya mahakama ya Jerusalem kukataa ombi lake kwamba hana akili timamu.

Mahakama imeamua Yosef Haim Ben-David alifahamu kikamilifu kuhusu vitendo vyake alipojihusisha na uhalifu huo. Gazeti la Haaretz limeripoti kwamba hukumu dhidi ya mshukiwa mkuu katika tukio la kuchomwa moto Mohammed Abu Khdair aliyekuwa na umri wa miaka 16, itatolewa siku nyingine.

Jerusalem Prozess Verurteilung Yosef Haim Ben David
Haim Ben David, anayetuhumiwa kwa kumuua MpalestinaPicha: picture alliance/AA/M. Awad

Vijana wawili waliokuwa na umri wa chini ya miaka 18 walipatikana na hatia Februari mwaka huu kwa kuhusika na tukio hilo mjini Jerusalem, ambalo likuwa mojawapo ya sababu zilizochochea mahafuko kabla kuanza vita vya Gaza 2014 kati ya Israel na Hamas. Vijana hao walihukumiwa kifungo cha maisha na miaka 21 gerezani mtawalia.

Wayahadui watatu wenye misimamo mikali ya kidini walikiri walitaka kulipiza kisasi utekaji nyara wa Juni 2014 na kuuliwa kwa vijana watatu wa Kiisraeli na Wapalestina. Waendesha mashitka walisema Ben-David alipanga kufanya uhalifu huo, huku vijana wengine wawili, ambao sasa wametimiza umri wa miaka 18, wakimsaidia.

Mwandishi:Josephat Charo/ape/rtre/afpe

Mhariri:Saumu Yusuf