1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu 30 wauwawa kwa kuchomwa moto kanisani.

2 Januari 2008
https://p.dw.com/p/CizZ

Nairobi. Kiasi watu zaidi ya 30 wameuwawa na wengine kadha wamejeruhiwa baada ya kundi la watu kuchoma moto kanisa magharibi mwa Kenya. Watu walioshuhudia wamesema kuwa watu kadha ikiwa ni pamoja na watoto wamechomwa moto ama kukatwakatwa mapanga hadi kufa katika ghasia za kikabila kufuatia matokeo ya uchaguzi mkuu wa Kenya yenye utata. Mauaji ya watu zaidi ya 50 wa kabila la Kikuyu katika mji wa bonde la ufa wa Eldoret jana Jumanne umefikisha idadi ya watu waliouwawa kutokana na siku nne za ghasia kuwa zaidi ya 275.

Vijana wakiwa na mapanga wameweka vizuizi barabarani nchini Kenya wakati nchi kadha za dunia zinaongeza juhudi zao za kumaliza wimbi la machafuko ya kikabila ambayo yanatishia kuivuruga nchi hiyo.

Akichangia kuongeza juu ya hali ya machafuko inayoendelea , mwenyekiti wa tume ya uchaguzi ya Kenya amenukuliwa akisema kuwa hafahamu iwapo rais Mwai Kibaki ameshinda uchaguzi. Maneno hayo ambayo inasemekana ameyatamka mwenyekiti wa tume hiyo Samuel Kivuitu, ambaye alitangaza siku ya Jumapili kuwa Kibaki amemshinda mgombea wa upinzani Raila Odinga , haijaweza kuthibitishwa mara moja.

Mwenyekiti wa umoja wa Afrika AU, anatarajiwa kufika nchini Kenya leo kwa mazungumzo ya dharura na rais Kibaki baada ya idadi ya vifo kukaribia 250 katika taifa hilo la Afrika mashariki.