1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu 35 wauawa kwenye mapigano kati ya jeshi na Al Shabaab

Zainab Aziz
5 Oktoba 2023

Takriban watu 35 wameuawa kwenye mapigano makali nchini Somalia kati ya vikosi vya kijeshi vya kikanda na wapiganaji wa kundi la kigaidi la Al-Shabaab.

https://p.dw.com/p/4X9MW
Somalia Anschlag | Explosion in Beledweyne
Picha: AP Photo/picture alliance

Kwa mujibu wa kamanda wa vikosi hivyo vya usalama, mapigano hayo yalidumu kwa saa kadhaa karibu na kijiji cha Shabelow, katika mkoa wa kati wa Somalia wa Mudug.

Zaidi ya wapiganaji 25 wa Al Shabaab na wanajeshi 10 wa upande wa serikali waliuawa. Naibu Waziri wa Habari wa Somalia Abdirahman Yusuf ameliambia shirika la Habari la Ujerumani dpa kuwa kundi la Al Shabaab limepata hasara kubwa na kwamba linapoteza maeneo zaidi kila kukicha.

Amesema uwepo wa kundi hilo katika jimbo la Galmudug la Somalia unaendelea kutoweka. Waziri Yusuf amesema wanajeshi wa Somalia, kwa msaada wa wanamgambo wa ndani, wamekuwa wanafanya mashambulizi makubwa dhidi ya wapiganaji wa Al-Shabaab.

Ameongeza kuwa wamefanikiwa pia kuyakomboa tena maeneo makubwa katikati mwa nchi, ambayo yalikuwa yanadhibitiwa na kundi la Al-Shabaab ingawa bado wapiganaji hao wa Al Shabaab wanadhibiti maeneo muhimu kusini mwa Somalia.