1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hali inazidi kuwa mbaya, watu 46 wajeruhiwa.

14 Mei 2010

Waziri mkuu wa zamani wa Thailand, Thaksin Shinawatra atoa mwito kwa serikali ianze tena mazungumzo ya amani.

https://p.dw.com/p/NO9M
Wanajeshi watumia vitoa machozi kuwatawanya waandamanaji mjini Bangkok.Picha: AP

Waandamanaji wa mashati mekundu wanaojaribu kuiangusha serikali ya waziri mkuu, Abhisit Vejjajiva walivurumusha mawe na kuripua fataki dhidi ya wanajeshi. Waandishi watatu wa habari, mmoja wao akiwa mfanyakazi wa shirika la habari la France 24, walifyatuliwa risasi miguuni walipokuwa kazini.

Wanajeshi walitumia vitoa machozi kuwatawanya waandamanaji walioteketeza magurudumu barabarani, wakatia moto basi la polisi na kuyapora magari ya wanajeshi ikiwemo moja ya kunyunyiza maji katika jitihada za kuvuruga mikakati ya kijeshi dhidi yao.

Unruhe und Gewalt in Thailand Flash-Galerie
Hali ya wasiwasi yatanda mjini Bangkok. Wanajeshi wanaendelea kupiga doria.Picha: AP

Leo alasiri milio ya risasi ilisikika mjini Bangkok na kusababisha waandamanaji kutawanyika huku hali ya wasiwasi ikitanda. Kulingana na mwandishi wa habari wa shirika la AFP, wanajeshi waliwashambulia waandamanaji kwa kufyatua risasi kabla ya kupanda kwenye mlima barabarani na kuanza kufyatua risasi hewani.

Mkurugenzi wa hospitali ilikopelekwa miili ya watu wawili, alisema walionekana kuwa walinzi wa waandamanaji hao wa mashati mekundu na mmoja alipigwa risasi kichwani na mwingine kifuani. Maiti ya tatu ilikuwa ya mtu wa umri wa miaka 32 aliyefariki kutokana na vidonda vya risasi.

Kiasi ya watu 33 wameuawa na wengine takriban 1000 kujeruhiwa mjini Bangkok katika msururu wa makabiliano na mashambulio tangu maandamano yaanze mwezi machi.

Hali ya wasiwasi imetanda katika eneo lililozingirwa na wanajeshi. Kiongozi wa ngazi ya juu wa waandamanaji hao, Nattawut Saikuar aliwambia waandishi wa habari kwamba waziri mkuu, Abhisit Vejjajiva tayari ameanzisha vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Saikuar alisema wanaitaka serikali iwaondoe wanajeshi na isitishe machafuko hayo. Aliongeza kwamba hajui jinsi watakavyoimudu hali ya mambo usiku wa leo ikiwa waziri mkuu atakataa kusitisha hatua hiyo ya wanajeshi .

Theluthi moja ya Thailand ukiwemo mji mkuu Bangkok iko chini ya sheria ya hali ya hatari.

Mwandishi, Peter Moss /AFP

Mhariri, Abdul-Rahman Mohammed