1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUgiriki

Watu 500 wahofiwa kufariki katika ajali ya boti Ugiriki

15 Juni 2023

Mamlaka za Ugiriki zimesema zinaamini kuwa zaidi ya watu 500 wamekufa baada ya boti ya wahamiaji kupinduka, na ripoti za vyombo vya habari vya ndani vikisema kwamba wengi wa waliofariki wanaweza kuwa watoto.

https://p.dw.com/p/4ScLD
Griechenland | Schiffsunglück bei Kalamata
Picha: Stelios Misinas/REUTERS

Inaarifiwa kuwa watu 104 wamenusurika katika ajali hiyo iliyotokea umbali wa kilomita 90 kutoka eneo la pwani ya kusini-magharibi ya Ugiriki siku ya Jumatano na kupelekwa katika kambi ya wakimbizi karibu na Athens.

Soma pia: Ugiriki yaendelea kusaka manusura wa boti iliyozama

Kulingana na mamlaka takriban watu 30 wamelazwa hospitalini wakiwa na homa ya mapafu na uchovu lakini hawako katika hatari.

Wakati jamaa katika nchi wanazotoka wahamiaji hao wakitafuta maelezo ya wapendwa wao, walinzi wa pwani walisema miili 78 na sampuli za vinasaba vya DNA zitachukuliwa ili kutambua miili hiyo. Juhudi za utafutaji ziliendelea usiku kucha na kuendelea siku ya Alhamisi, lakini bila mafanikio.

Soma pia: Wahamiaji 59 wafa maji, wengine kadhaa hawajulikani walipo baada ya boti ya uvuvi kupinduka na kuzama Ugiriki

Kulingana na simulizi za manusura wa mkasa huo baadhi yao wamekadiria kwamba boti hiyo huenda iliwabeba zaidi ya watu 700 na takriban watoto 100.

Akizungumza na shirika la utangazaji la serikali ERT, Stella Nanou kutoka shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia wakimbizi la UNHCR amesema "Hili linaweza kuwa janga baya zaidi la baharini nchini Ugirikikatika miaka ya hivi karibuni.

Msemaji wa walinzi wa pwani ya Ugiriki amesema  kwamba hakuna manusura wala waathiriwa zaidi waliopatikana wakati wa operesheni hiyo usiku kucha na inadhaniwa kuwa watu waliokuwa juu ya boti hilo hawakuweza kujiokoa wenyewe wakati chombo hicho cha urefu wa mita 30, kilichokuwa na kutu kilipozama.

Akizungumza wakati wa opereshini hiyo mkurugenzi wa afya wa mkoa Giannis Karvelis, amesema "Kwa hakika ni operesheni kubwa kwa sababu tunazungumzia kuhusu idadi kubwa sana ya watu waliozama. Nadhani ni mojawapo ya zoezi gumu na kubwa zaidi katika suala la idadi ya watu waliozama ambalo taifa la Ugiriki limekabiliana nalo hadi sasa."

Abiria walikataa usaidizi

Griechenland Schiffsunglück
Picha: HELLENIC COAST GUARD/REUTERS

Kwa mujibu wa mlinzi wa pwani ndege ya uchunguzi ya Shirika la Ulinzi wa Mipakani la Umoja wa Ulaya, Frontex iliiona boti hiyo Jumanne mchana, lakini abiria walikataa msaada wowote. Injini ya mashua iliacha kufanya kazi muda mfupi kabla ya tano usiku siku ya Jumanne na meli hiyo ilizama kwenye kina kirefu cha maji ndani ya dakika 10 hadi 15.

Msemaji wa serikali Ilias Siakantaris jana Jumatano alisema hakuna mtu kwenye boti hilo alikuwa amevaa jaketi la kuokoa maisha.

Soma pia: Wahamiaji 2 wafariki, wengine 20 hawajulikani walipo baada ya ajali ya boti huko pwani ya Italia

Mamlaka ilisema inaonekana wahamiaji hao walikuwa wametokea Libya na walikuwa wakielekea Italia. Walionusurika zaidi ni kutoka Syria, Misri na Pakistan, na wamehifadhiwa kwa muda katika bohari la bandari ili kutambuliwa na kuhojiwa na mamlaka ya Ugiriki, ambayo inatafuta uwezekano wa wasafirishaji kati yao.  

Watu wanane wanahojiwa kuhusiana na ajali hiyo. Kaimu waziri wa uhamiaji Daniel Esdras aliiambia ERT kwamba walionusurika watapelekwa kwenye kambi ya wahamiaji karibu na Athens na watachunguza madai yao ya kuomba hifadhi, lakini watakaobainika kuwa hawana haki ya kulindwa watarejeshwa nyumbani.