1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu 62 wanamiliki nusu ya utajiri wa dunia

Admin.WagnerD18 Januari 2016

Matajiri zaidi 62 duniani, hivi sasa wanamiliki zaidi ya nusu ya utajiri wa wakaazi wote wa dunia, limesema shirika la hisani la Oxfam, kuelekea mkutano wa kiuchumi wa dunia - World Economi Forum (WEF) Davos, Uswis.

https://p.dw.com/p/1HfFO
Davos Weltwirtschaftsforum 2016

Ripoti hiyo ya Oxfam inasema utajiri wa watu hao 62 matajiri zaidi umeongezeka kwa asilimia 44 tangu mwaka 2010, huku utajiri wa watu maskini zaidi bilioni 3.5 umeshuka kwa asilimia 41. Ripoti hiyo iliyopewa kichwa cha habari kisemacho: "Uchumi wa asilimia 1", inabainisha kuwa wanawake wanaathirika zaidi na ukosefu wa usawa duniani.

Karibu nusu ya matajiri zaidi wa dunia wanatokea nchini Marekani, 17 barani Ulaya na waliosalia wanatoka katika mataifa yakiwemo China, Brazil, Mexico, Japan na Saudi Arabia.

Moja ya mambo muhimu yaliyoainishwa katika ripoti ya Oxfam ambayo yanayochangia ukosefu wa usawa duniani ni kupungua kwa mgao wa pato la taifa linalokwenda kwa wafanyakazi karibu katika mataifa yote yalioendelea na yanayoendelea, na kuongeza kuwa wengi wa wafanyakazi wanaolipwa kiasi kidogo zaidi cha mshahara ni wanawake.

Wanaharakti wa Oxfam wakiwa wameva vikaragis vya baadhi ya viongozi wa Dunia watakaoshiriki mkutano wa WEF.
Wanaharakti wa Oxfam wakiwa wameva vikaragis vya baadhi ya viongozi wa Dunia watakaoshiriki mkutano wa WEF.Picha: C. Stache/AFP/Getty Images

Pengo la walio na wasio nacho lazidi kupanuka

Ingawa viongozi wa dunia wamezidi kuzungumzia haja ya kukabiliana na ukosefu wa usawa, Oxfam inasema pengo kati ya matajiri zaidi na wengine limetanuka zaidi katika kipidi cha miezi 12 iliyopita.

Utabiri wa Oxfam, yaliyotolewa siku moja kuelekea mkutano wa Davos wa mwaka jana - kwamba asilimia moja ya matajiri zaidi wa dunia watamiliki zaidi ya sisi sote tuliobakia katika muda usiyo mrefu, ulitimia mwaka 2015, imeongeza ripoti hiyo.

Wakati idadi ya watu wanaoishi katika hali ya umaskini uliyokithiri ilipingua kwa nusu kati ya mwaka 1990 na 2010, wastani wa kipato cha asilimia 10 ya watu maskini zaidi duniani umeongezeka kwa chini ya dola tatu kwa mwaka katika kipindi cha robo karne iliyopita, hili likiwa ongezeko la chini ya senti moja katika kipato cha mtu mmoja mmoja kwa mwaka.

Zaidi ya wakuu 40 wa nchi na serikali watahudghuria mkutano wa Davos unaoanza Jumanne jioni na kumalizika Januari 23. Taarifa ya awali iliyotolewa na waandaji wa mkutano huo wa uchumi duniani, ilisema mkutano huo wa ngazi ya juu unaofanyika katika eneo la mapumziko la Davos nchini Uswisi watahusisha pia viongozi wapatao 2,500 wa kibiashara na kijamii.

Mwasisi wa mkutano wa WEF, Mjerumani Klaus Schwab.
Mwasisi wa mkutano wa WEF, Mjerumani Klaus Schwab.Picha: Reuters/P. Albouy

Mapinduzi ya nne ya kiviwanda

Akifafanua kuhusu kaulimbiu ya mwaka huu -- Mapinduzi ya nne ya kiviwanda -- mwasisi wa WEF Klaus Schwab amesema inamaanisha kuunganisha teknolojia katika ulimwengu wa kimaumbile, kidigitali na kibayolojia, ambako kunaanzisha uwezo mpya kabisaa na kuathiri mifumo ya kisiasa, kijamii na kiuchumi.

Mkurugenzi mkuu wa shirika la Oxfam Winnie Byanyima, ambaye anahudhuria mkutano wa Davos baada ya kuwa mwenyekiti mwenza wa mkutano wa mwaka uliyopita, alisema haikubaliki kwa nusu ya watu maskini zaidi wa dunia kumiliki siyo zaidi ya matajiri zaidi wachache, ambao wanaweza kuingia katika basi moja.

Utajiri wa Afrika nje

Kama kipaumbele, Oxfam inataka kukomeshwa kwa enzi ya maeneo salama ya kodi, ambao yameshuhudia ongezeko la matumizi ya vituo vya nje kukwepa kulipa kodi. "Hili linazinyima serikali rasilimali muhimu zinahitajika kupambana na umaskini na ukosefu wa usawa," inasema ripoti hiyo.

Karibu asimilia 30 ya utajiri wa kifedha wa Afrika unakadiriwa kushikiliwa nje ya bara hilo, iliongeza ripoti hiyo, na hivyo kugharimu takribani dola bilioni 14 katika mapato yanayopotezwa kila mwaka.

Wanaharakati wa Oxfam wakiandama kupinga ukosefu wa usawa wa kiuchumi.
Wanaharakati wa Oxfam wakiandama kupinga ukosefu wa usawa wa kiuchumi.Picha: picture-alliance/dpa

Kufikia viwango sahihi vya kodi kutakuwa muhimu ikiwa viongozi wa dunia watafikia malengo yao, waliojiwekea mwaka uliyopita, ya kufuta kabisaa umaskini uliyokithiri ifikapo mwaka 2030.

Byanyima aliwapa changamoto washiriki wa mkutano wa Davos kutoa mchango wao katika kukomesha enzi ya maeneo salama ya kodi, ambayo yanachochea ukosefu wa usawa wa kiuchumi na kuwazuwia mamia ya mamilioni ya watu kujiondoa katika umaskini.

Miongoni mwa watu 62 wanaosemekana kumiliki utajiri sawa na asilimia 50 ya maskini zaii, Oxfam ilisema 53 ni wanaume na tisa tu ndiyo wanawake, hii ikionyesha kuwa hata kwenye ngazi za juu wanawake wanawakilishwa vibaya.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/afpe,rtre
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman