1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu saba wauwawa katika msururu wa mashambulizi ya bomu Nigeria

21 Januari 2012

Msururu wa miripuko ya bomu iliyoratibiwa na mashambulizi ya bunduki yanayodaiwa kufanywa na kundi la Boko Haram, yameua watu saba katika mji wa Kano, ulio mkubwa kabisa kaskazini mwa Nigeria na wenye waislaamu wengi.

https://p.dw.com/p/13nW4
Eneo la mlipuko wa bomu nchini Nigeria
Eneo la mlipuko wa bomu nchini NigeriaPicha: DW

Mashambulio hayo yanatishia kulitumbukiza eneo zima katika machafuko.
Milio ya risasi ilisikika katika mji huo wa Kano jana usiku, huku maafisa wa usalama wakiwaondoa maafisa wa huduma za dharura kutoka maeneo ya mashambulizi. Kiwango cha mashambulizi hayo kilionyesha uwezekano wa kuongezeka idadi ya vifo. Vile vile ni shambulizi kuu la kwanza kufanywa na wanachama wa kundi la Boko Haram katika mji wa Kano, ulio na zaidi ya watu milioni 9, wakiwemo viongozi wengi maarufu wa kisiasa na kidini ambao ni kwa waislamu nchini Nigeria.

Mashambulizi hayo yalianza mwendo wa saa kumi na moja jioni, baada ya sala ya mchana wakati wafanyakazi walipoanza kuondoka ofisini kurejea makwao. Mwandishi wa habari wa shirika la AP amesema, mripuko mkubwa uliotokea katika makao makuu ya polisi uliyatikisa magari yaliyokuwa umbali wa maili kadhaa kutoka eneo hilo. Naibu mkuu wa polisi, Aminu Ringim amesema, shambulio hilo lilifanywa na mshambuliaji aliejitoa mhanga, ambaye aliendesha gari hadi ndani ya uwanja wa kituo cha polisi na kuyaripua mabomu yake.

Serikali imetangaza amri ya kutotoka nje saa 24

Afisa wa kitengo cha kitaifa cha maswala ya dharura nchini Nigeria Abubakar Jibril, amesema ,miripuko mitatu ililenga vituo vingine vitatu vya polisi katika mji huo, huku milio ya risasi ikisikika barabarani. Mripuko mwingine, ulilenga makao makuu ya huduma za usalama. Walioshuhudia wamesema, wafungwa katika kituo cha polisi cha eneo hilo walitoroka wakati wa milio hiyo ya risasi. Vile vile wameona maiti za polisi watatu na mwandishi habari mmoja. Serikali imetangaza amri ya kutotoka nje saa 24, huku wakaazi wakijificha ndani ya nyumba zao wakati mapigano yakiendelea. Msemaji wa Boko Haram aliejiita Abul Qaga, alidai kuhusika na mashambulizi hayo. Alisema, walifanya mashambulizi hayo kwa sababu serikali imekataa kuwaachia wanachama wa Boko Haram wanaozuliwa na polisi.

Mwandishi: Bruce Amani/AP
Mhariri: Martin, Prema

Wanawake wakiomboleza vifo vya wapendwa wao
Wanawake wakiomboleza vifo vya wapendwa waoPicha: Reuters