1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu saba wauwawa Kenya huku juhudi za upatanishi zikiendelea

25 Januari 2008
https://p.dw.com/p/CxcE

Watu saba wameuwawa magharibi mwa Kenya huku katibu mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa, Kofi Annan, akiendelea na juhudi za mazungumzo kati ya mahasimu wawili wa kisiasa nchini humo.

Duru za polisi zinasema watu watano wamechinjwa na kuuwawa mjini Molo na Nakuru katika mkoa wa bonde la ufa. Kamanda wa polisi mkoani humo amesema watu wengine wawili, akiwemo kijana wa umri wa miaka 13, wamepigwa risasi na kuuwawa mjini Molo.

Hii leo aliyekuwa zamani katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Kofi Annan, anakutana tena na rais Mwai Kibaki na kiongozi wa upinzani, Raila Odinga, mjini Nairobi kujaribu kuutanzua mgogoro wa kisiasa ambao umekuwa ukiendelea nchini Kenya tangu kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi wa mwaka jana.

Bwana Kofi Annan alifaulu jana kwa mara ya kwanza kuwakutanisha rais Kibaki na mheshimiwa Odinga. Raila Odinga amesema atafanya kila jitihada kuhakikisha makubaliano yanafikiwa na upande wa rais Kibaki.

Mgombea urais nchini Marekani, Barack Obama, amesema kukutana kwa rais Kibaki na Raila Odinga ni nafasi ya mwanzo mpya. Obama amesema mazungumzo hayo ni hatua ya kwanza tu lakini viongozi wote wawili wanatakiwa waendelee na mazungumzo bila masharti ili wafikie suluhisho la kisiasa la mzozo uliopo.

Waziri wa mashauri ya kigeni wa Nigeria, Ojo Madueke, leo amewatolea mwito viongozi wa kisiasa nchini Kenya wajizuie kufanya machafuko na wawasilishe malalamiko yao katika taasisi za kisheria.