1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu takriban 14 waungua hadi kufa mjini Naivasha Kenya

Josephat Charo28 Januari 2008

Konare atoa mwito mzozo wa kisiasa nchini Kenya utatuliwe

https://p.dw.com/p/CyXl
Wakaazi wa Naivasha wakikimbia machafuko ya kikabila Jumapili tarehe 27 JanuariPicha: AP

Watu takriban 14 waliungua hadi kufa hapo jana wakati walipokuwa wakijificha kutokana na machafuko ndani ya nyumba moja mjini Niavasha magharibi mwa Kenya.

Watu wengine tisa waliuwawa hapo kabla wakati wa mapambano makali kati ya magenge ya vijana kutoka maeneo ya madongo poromoka mjini humo.

Idadi ya watu waliouwawa magharibi mwa mkoa wa bonde la ufa imefikia 130 tangu Alhamisi wiki iliyopita.

Mauji yanayoendelea nchini Kenya yanadumaza juhudi za katibu mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa Kofi Annan kujaribu kuutanzua mzozo wa kisiasa nchini Kenya uliosababishwa na matokeo ya uchaguzi wa mwaka jana.

Akiwa katika siku yake ya sita ya ziara yake nchini humo Kofi Annan jana alikutana na kiongozi wa upinzani Raila Odinga ambaye amelaani vikali mauaji yanayoendelea huko Naivasha.

Odinga amedai makundi ya wahalifu yanayolindwa na polisi yanawaua watu bila kujali.

Wakati huo huo, katibu mkuu wa Umoja wa Afrika, Alpha Oumar Konare, ametoa mwito mzozo wa kisiasa nchini Kenya utafutiwe ufumbuzi.

Kiongozi huyo ameelezea wasiwasi wake kuhusu machafuko yanayoendelea nchini humo yaliyosababishwa na matokeo ya uchaguzi wa tarehe 27 mwezi Disemba mwaka jana.

Akizungumzia ujumbe wa aliyekuwa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Kofi Annan, kuhusu ukiukaji wa haki za binadamu, bwana Konare amewataka viongozi wajiulize kuhusu jukumu la Rwanda katika mauaji ya halaiki ya mwaka wa 1994 ambapo wanyarwanda takriban laki nane waliuwawa.

Konare alikuwa akizungumza kwenye mkutano wa mawaziri wa mashauri ya kigeni wa Umoja wa Afrika wanaokutana mjini Addis Abba nchini Ethiopia kabla kuanza kwa mkutano wa kilele wa nmoja huo Alhamisi ijayo mjini humo.

Huku akiutaka umoja wa Afrika uisaidie Kenya, Konare amesema suluhisho si kugawana madaraka bali kuiheshimu misingi ya utawala bora na kukabiliana na machafuko.