1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu takriban 17 wafa maji nchini Kongo

31 Januari 2008
https://p.dw.com/p/D05c

Watu takriban 17, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, wamekufa maji nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wakati feri waliyokuwa wakisafiria ilipozama katika ziwa Tanganyika. Watu wengine wasiopungua 120 wamenusurika.

Manusura hao aidha waliogelea hadi ufuoni au kuokolewa baada ya feri hiyo kuzama Ijumaa wiki iliyopita wakati ilipogonga mwamba yapata kilomita tano kusini mwa mji wa Kalemie karibu na ziwa Tanganyika katika mpaka wa mashariki wa Kongo na Tanzania.

Imechukua siku kadhaa kabla taarifa za ajali hiyo kufika mjini Kinshasa.

Sambamba na hayo Umoja wa Mataifa umejenga kambi nane mpya za jeshi lake mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia Kongo kusimamia mkataba wa usitishwaji mapigano uliosainiwa hivi majuzi kati ya jeshi la Kongo na waasi.

Msemaji wa tume ya kulinda amani nchini Kongo, MONUC, luteni kanali Jean Paul Dietrich, amesema kambi hizo zitatumiwa na vikosi 30 vitakavyowalinda pia wakaazi wa mkoa wa Kivu Kaskazini.