1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu wa Darfur wapiga kura ya maoni

12 Aprili 2016

Wakazi wa eneo la Darfur nchini Sudan wanapiga kura Leo ya maoni Leo, ambayo inasusiwa na waasi. Kura hiyo inahusu iwapo majimbo matano ya Darfur yaunganishwe katika jimbo moja au yaendelee yalivyo kwa sasa.

https://p.dw.com/p/1IT7H
Kura hii ya maoni Darfur imesusiwa na upande wa waasi.
Kura hii ya maoni Darfur imesusiwa na upande wa waasi.Picha: AFP/Getty Images/P. Baz

Waandishi wa habari katika eneo hilo la Darfur linalokabiliwa na machafuko, wanasema zoezi la upigaji kura limeanza saa tatu majira ya mahali hapo.

Makundi ya waasi wanaotoka jamii za wachache katika jimbo hilo, kwa muda mrefu wamekuwa wakitaka eneo la Darfur liunganishwe tena katika jimbo moja, kama ilivyokuwa hadi mwaka 1994. Baada ya mwaka huo serikali ya Khartoum iliigawa Darfur katika majimbo matatu, na baadaye mwaka 2012, ikaligawa zaidi na kufikisha majimbo matano.

Serikali ya rais Omar al-Bashir inasema kuligawa eneo hilo katika majimbo madogo kunarahisisha shughuli za kiuongozi na huduma kwa wananchi, lakini waasi wanaotaka mamlaka zaidi ndani ya jimbo lao, wanasema kuligawa kumeiwezesha serikali kuu kulidhibiti kirahisi.

Waasi wahofia mizengwe

Makundi hayo ya waasi yamesusia kura ya maoni ya leo, yakisema kura hiyo haiwezi kuwa huru wala ya haki kwa sababu ya mapigano yanayoendelea. Mapigano makali baina ya waasi na vikosi vya serikali katika milima ya Marra katikati mwa Darfur, yamewalazimisha zaidi ya watu 100,000 kuyahama makazi yao tangu mwezi Januari mwaka huu, hii ikiwa ni kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa.

Rais wa Sudan, Omar al-Bashir, ameamuru kura ipigwe kama ilivyopangwa
Rais wa Sudan, Omar al-Bashir, ameamuru kura ipigwe kama ilivyopangwaPicha: Reuters

Akizungumza wiki iliyopita, rais al-Bashiri alisema na hapa namnukuu, ''Ni jukumu la watu wa Darfur kuamua kuwa na jimbo moja au majimbo mengi, na tunaendesha kura hii ya maoni, ili asiwepo mtu mwingine anayesema, tunataka hiki au kile'', mwisho wa kumnukuu.

Marekani yaelezea wasiwasi

Kauli hiyo ya rais Bashir imepinga na Marekani, ambayo imeelezea hofu kuwa kura hiyo ya maoni inaweza kuathiri vibaya mchakato wa amani ambao unaendelea kwa wakti huu. Msemaji wa wizara ya mambo ya nchi za nje ya Marekani Mark Toner, amesema kwa kufanyika katika mazingira ya sasa jimboni Darfur, kura hiyo haiwezi kuchukuliwa kama yenye kuwakilisha matakwa ya watu wa jimbo hilo.

Vita vya muda mrefu vimewafanya wakazi wengi wa Darfur kukimbilia katika makambi ya ndani ya nchi
Vita vya muda mrefu vimewafanya wakazi wengi wa Darfur kukimbilia katika makambi ya ndani ya nchiPicha: picture-alliance/AP Photo/K. Prinsloo

Bado haijulikani namna watu walio katika makambi ya walioyahama makazi yao, ambao wengi ni wapinzani wa serikali ya Khartoum, wanatakavyopiga kura hiyo.

Mchambuzi wa masuala ya siasa Magdi al-Gizouli anasema kuiendesha kura hiyo, huku serikali ikiwa inayadhibiti maeneo makubwa ya Darfur na uwezo mkubwa wa kufanya kampeni, kunaweza pia kuwa na makusudi ya kuyadhoofisha matakwa ya waasi kutaka Darfur iliyoungana na yenye utawala wa ndani.

Naye Abdullah Mursal, kiongozi wa tawi la kijeshi la kundi la Sudan Liberation Army linaloongozwa na Minni Minnawi, amesema ingawa kura ya maoni inayopigwa leo inatambuliwa kikatiba, sio suala lenye kipaumbele, na kuongeza kuwa serikali ya Khartoum inaonekana kuliweka mbele ya masuala muhimu zaidi yaliyoafikiwa katika makubaliano ya amani ya Doha.

Mwandishi: Daniel Gakuba/afpe

Mhariri:Iddi Ssessanga