1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu wanane wauawa Kabul, 100 wajeruhiwa

7 Agosti 2015

Mripuko wa bomu lenye nguvu lililotegwa kwenye gari leo hii umesababisha vifo vya watu wanane na wengine zaidi ya 100 kujeruhiwa, mjini Kabul, Afghanistan

https://p.dw.com/p/1GBX5
Afghanistan Kabul Selbstmordanschlag Autobombe
Eneo lililotokea mripuko la Afghanistan mjini Kabul.Picha: Reuters/Ahmad Masood

Hilo ni shambulio la kwanza, kubwa kufanyika katika maeneo ya mji mkuu wa Afghanistan, Kabul tangu kutangazwa kwa kifo cha kiongozi wa Taliban Mullah Omar.

Mpaka sasa hakuna kundi lilijinasibu kuhusika na shambulio hilo ambalo linafanyika wakati kundi la Taliban likijipanga katika kufanya mashambulizi yake katika kipindi cha kiangazi huku likiwa katika makali ya kubadilisha uongozi katika harakati zao.

Wanawake na watoto ni miongoni mwa waliouwawa katika shambulio hilo kubwa lililotokea katika kitongoji cha Shah Shaheed, mashariki mwa mji wa Kabul, lakini mzizimo wake ulisikika katika maeneo yote ya mji, kuharibu majengo, madirisha ya nyumba. Shambulio hilo limeacha mashimo, katika maeneo ya barabara, kiasi cha kina futi 30, na kuyageuza maeneo ya mbele ya majengu kuwa kifusi.

Idadi ya waliokufa inaweza kuongezeka

Msemaji wa jeshi la polisi mjini Kabul Ebadullah Karimi, ameliambia shirika la habari la IPS kwamba "Idadi ya watu waliokufa imefikia wanane, na majeruhi 128,"

Local Heroes Netzwerk Blutspende Your Blood My Life
Watu wakijitolea kuchangia damuPicha: DW/H. Sirat

Mkuu wa jeshi hilo mjini Kabul Abdul Rahman Rahimi vilevile amethibitisha idadi hiyo ya waliokufa na kujeruhiwa na kuongeza polisi inaendelea na jitihada za kuwasaka walionasa kwenye vifusi au kuporomokewa na zege katika majengo yaliobomoka. Amesema lengo la shambulio hilo lilikuwa kufanya mauwaji ya halaiki.

Msemaji wa wizara ya Afya Wahidiullah Mayar amesema idadi kubwa ya waliojeruhiwa inayokaribia watu 100 wanauguza majeraha yaliotokana na kukatwa na vioo vilivyopasuka.

Hata hivyo bado haijaweza kuwa wazi kama shambulio hilo lilikuwa likilenga kambi ya jeshi la taifa la Afganistan iliyopo karibu na Shah Shaheed, sehemu yenye idadi kubwa ya raia wa kipato cha wastani pasipo raia wa kigeni, lakini Rahimi amesema hakuna athari zilitoripotiwa kwa upande wa jeshi.

Mayar kutoka wizara ya afya amesema majeruhi wanapatiwa matibabu katika hospitali za jiji, ambapo kumeibuka ripoti za kuibuka kwa tatizo la uhaba wa damu na kutolewa ombi katika mitandao ya jamii kwa jamii kujitolewa katika kuchangia kutatua tatizo hilo.

Mashambulizi zaidi ya Talibani

Mauwaji hayo makubwa yanatokea siku moja tu, baada ya Wanamgambo wa Taliban kuwauwa watu tisa katika matukio kadhaa ya kuwalenga polisi katika maeneo ya kusini na mashariki mwa Afghanistan.

Mshambulizi haya ya sasa yanaonesha wazi kuongezeka hali ya kutokuwepo kwa usalama huku kukigubikwa na kusuasua mchakato wa amani kwa Taliban, wakati huohuo jeshi la Afghanistan likikabiliwa na mapambano ya mwanzo katika msimu huu ya kianganzi bila ya kuwepo kwa usaidizi wa jumuiya ya kujihami ya NATO.

NATO kwa upande wake imelaani shambulio la Afghanistan kwa kueleza kuwa ni " Vitendo vya vurugu visivyo na sababu yoyote"

Mwandishi: Sudi Mnette AFP
Mhariri: Iddi Ssessanga