1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu zaidi 20 wauwawa mkoa wa pwani Kenya

6 Julai 2014

Takriban watu 21 wameuwawa Jumamosi usiku katika mashambulizi kwenye kaunti mbili za mwambao wa Kenya ambapo polisi inawalaumu wanaharakati wanaotaka kujitenga katika mkoa wa pwani kuhusika na mashambulizi hayo.

https://p.dw.com/p/1CWcF
Lori lililoteketezwa nje ya kituo cha polisi cha Gamba.(06.07.2014)
Lori lililoteketezwa nje ya kituo cha polisi cha Gamba.(06.07.2014)Picha: picture alliance/dpa

Naibu Mkuu wa polisi wa Kenya Grace Kaindi amesema watu 21 wameuwawa katika mashambulizi hayo mawili ya usiku na kuwalaumu wanachama wa chama cha Mombasa Republican Council (MRC) kundi lenye kupigania uhuru wa mkoa wa pwani kwa kuhusika na mashambulizi hayo licha ya kundi la Al-Shabab la Somalia kudai kuwajibika na mashambulizi hayo.

Akizungumza na waandishi wa habari katika makao ya polisi mjini Nairobi Kaindi amekaririwa akisema "Uchunguzi wa awali unaonyesha shambulio hilo limefanywa na wanachama wa MRC."

Ameongeza kusema kuna ushahidi masuala hayo yamechochewa kisiasa na kidini.

Mauaji ya jana yametokea huko Hindi ilioko kilomita 15 kutoka kisiwa cha utalii cha Lamu katika kaunti ya Lamu na huko Gamba katika kaunti jirani ya Tana River. Hindi iko kilomita 40 kaskazini mwa Mpeketoni ambapo watu kadhaa waliuwawa katika shambulio la mwezi uliopita wakati Gamba iko kama kilomita 70 kaskazini magharibi mwa Mpeketoni.

Polisi imesema watu waliokuwa na silaha waliwauwa watu 13 huko Hindi na kuzitia moto nyumba kadhaa.Kamanda wa polisi wa mkoa wa pwani Robert Kitur ameliambia shirika la habari la Ujerumani dpa kwamba wale waliouwawa huko Hindi wamepigwa risasi na wengine kukatwa kwa mapanga.

Wasi wasi umetanda

Mmwakilishi wa shirika la Msalaba Mwekundu la Kenya amesema miongoni mwa waliouwawa ni mwanaume ambaye nusu ya mwili wake ulikuwa umeunguwa na mwanawe wa kiume ambaye alivuja damu baada ya kupigwa risasi kwenye kiwiko.

Steven Kang'ethe akipatiwa matibabu baada ya kupigwa risasi katika kijiji cha Hindi. (06.07.2014)
Steven Kang'ethe akipatiwa matibabu baada ya kupigwa risasi katika kijiji cha Hindi. (06.07.2014)Picha: Reuters

Mwakilishi huyo wa Shirika la Msalaba Mwekundu ambaye alikataa kutajwa jina lake amesema kuna hali ya wasi wasi mkubwa na kwamba watu wanaonekana kuyahama mashamba yao na hadhani iwapo watu hao wataweza kuendelea kubakia wakati wa usiku.

Huko Gamba washambuliaji hao walikishambulia kituo cha polisi ambapo walipambana vikali na polisi.Mwakilishi huyo wa Shirika la Msalaba Mwekundu amesema watu tisa wameuwawa huko Gamba.

Polisi mmoja auwawa

Gazeti la Daily Nation limemkariri Naibu Kamishna wa Polisi Mike Kimoko akisema kwamba washambuliaji hao walimuuwa polisi mmoja yaliyekuwa zamu kabla ya kuwafungulia watu watano waliokuwa mahabusu na kuwauwa kwa kuwapiga risasi.

Polisi na maafisa wa Shirika la Msalaba Mwekundu katika eneo lililoshambuliwa la Gamba.(06.07.2014)
Polisi na maafisa wa Shirika la Msalaba Mwekundu katika eneo lililoshambuliwa la Gamba.(06.07.2014)Picha: picture alliance/AP Photo

Walimuachilia anayetuhumiwa kuwa kiongozi wa shambulio kama hilo la Mpeketoni karibu na Hindi ambapo zaidi ya watu 60 waliuwawa hapo mwezi wa Juni.Polisi watano walijeruhiwa katika shambulio hilo na mmoja ameuwawa.

Gazeti hilo la Daily Nation pia limeripoti kwamba washambuliaji hao waliwateremsha kwenye lori raia watatu ambao ndio kwanza walikuwa wamewasili katika kituo hicho cha polisi na kuwauwa kabla ya kutoweka kichakani.Kitur amesema polisi inawasaka wauawaji hao.

Shambulio la Hindi linakuja wakati Makamu wa Rais William Ruto akiutembelea mkoa wa pwani ambapo leo alitarajiwa kuitembelea Mpeketoni kuhudhuria mkutano wa sala ya maombi.

Mkono wa Al-Shabab au wanasiasa?

Kundi la itikadi kali la Kiislamu la Al Shabab la Somalia limedai kuhusika na mashambulizi ya Mpeketoni, lakini Rais Uhuru Kenyatta amewalaumu wapinzani wake wa kisiasa kwa kuwa na mkono wao katika mashambulizi hayo.

Mwanakijiji nje ya nyumba ilioharibiwa kufuatia shambulio la kijiji cha Hindi. (06.07.2014)
Mwanakijiji nje ya nyumba ilioharibiwa kufuatia shambulio la kijiji cha Hindi. (06.07.2014)Picha: Reuters

Mwishoni mwa mwezi uliopita polisi ilimkamata Gavana wa Lamu Issa Timammy na kumfungulia mashtaka ya mauaji, kuhusika kuhamishwa watu kwa nguvu pamoja na mashtaka ya ugaidi kuhusiana na mashambulizi ya Mpeketoni.

Al-Shabab imekuwa ikifanya mashambulizi nchini Kenya tokea nchi hiyo ilipotuma vikosi vyake nchini Somalia hapo mwaka 2011 kuisaidia serikali ya nchi hiyo kupambana na waasi.

Hapo mwezi wa Septemba mwaka jana Al-Shabab iliripua kwa mabomu jengo la maduka la Westgate mjini Nairobi na kuuwa watu 67.

Mashambulizi mengine madogo madogo yameuwa watu kadhaa katika kitongoji cha Wasomali mjini Nairobi,katika mji wa mwambao wa Mombasa na katika eneo la kaskazini mashariki karibu na mpaka na Somalia.

Mwandishi : Mohamed Dahman/ dpa/AP

Mhariri :Caro Robi

Ameongeza kusema kuna ushahidi