1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waumini wamuaga Papa

19 Februari 2013

Maelfu ya watu wamekusanyika katika uwanja wa kanisa la mtakatifu Petro wakihudhuria tukio la mwisho la baba mtakatifu Benedict wa 16 la kuwaombea waumini hadharani,

https://p.dw.com/p/17fjY
Papa Benedict wa 16 awaaga waumini,Vatican
Papa Benedict wa 16 awaaga waumini,VaticanPicha: picture-alliance/dpa

Hiyo ni  ibada ya mwisho ya baba mtakatifu ya mwisho ya hadhara ya siku ya Jumapili kabla ya kuachia kabisa nafasi hiyo ya kuliongoza kanisa katoliki duniani.

Kimsingi misa hiyo ya mchana ya jumapili huwavutia watu wachache ikiwa ni pamoja na watalii lakini mara hii wamejitokeza maelfu kwa maelfu ya waumini katika uwanja huo kumshuhudia kwa mara yao ya mwisho papa Benedict. Inasaidikiwa kwamba watu 150,000 wanahudhuria misa hiyo ya wazi katika uwanja wa mtakatifu Petro.

Waumini wa kanisa Katoliki
Waumini wa kanisa KatolikiPicha: Getty Images

Wamuaga

Baadhi ya watalii wamesikika kusema kwamba wamefika katika uwanja huo kumuaga na kumtakia mema na zaidi ya yote, mtalii kama Amy Champion aliyetokea Uingereza anasema inahitaji ujasiri kufanya kazi ya Papa na vile vile wakati unapoamua kuachia ngazi.

Kuanzia Jumapili Jioni baba mtakatifu hatoweza kuonekana tena mbele ya hadhara katika kipindi cha wiki nzima, ambacho kanisa mjini Vatican linaanza kipindi maalum cha maombi  na tafakari. Jumapili hii uongozi wa mji wa Roma uliongeza usafiri wa mabasi na Treni za chini kwa chini ili kusaidia kukabiliana na msongamano wa watu waliokuwa wanamiminika kuelekea Vatican pamoja na kutowa usafiri wa bure wa mabasi madogo kwa ajili ya wakongwe na walemavu.

Kujiuzulu kwake

Kiongozi wa kanisa Katoliki baba mtakatifu Benedict wa 16 aliushtuwa ulimwengu wiki iliyopita kwa kutangaza anajiuzulu kuanzia Februari 28, kitendo ambacho hakijawahi kushuhudiwa na kanisa hilo kwa kipindi cha miaka 600. Wakati Makadinali wakitazamiwa kumchagua mrithi wake mpya katika kikao maalum cha siri, baba mtakatifu Benedict mwenye umri wa miaka 85 atakuwa katika mapumziko na kufanya ibada katika makazi ya kanisa huko Kusini mashariki mwa mji wa Roma.

Bildergalerie Papst Benedikt XVI Rücktritt
Makadinali wakishauriana punde baada ya papa kujiuzulu tarehe 11 Februari 2013Picha: Reuters

Baada ya wiki kadhaa anatazamiwa kuhamia kwenye makaazi mengine yaliyoko kwenye eneo la Vatican ambako ataishi maisha ya kitawa. Makao makuu ya kanisa hilo Katoliki mjini Vatican hayajatangaza tarehe ya kuanza kwa kiao cha siri cha kumchagua kiongozi mpya lakini yametangaza kwamba kikao hicho huenda kikafanyika mapema kabla ya mwezi March 15 na tarehe hiyo mpya inaweza kutangazwa chini sheria za sasa za kanisa.

Papa Benedikt XVI katika misa ya Jumatano ya majivu Februari 13,2013
Papa Benedikt XVI katika misa ya Jumatano ya majivu Februari 13,2013Picha: Getty Images

Uchaguzi wa papa mpya

Papa atahitajika kutia saini juu ya tarehe hiyo kitendo ambacho kitakamilisha kabisa kipindi chake cha takriban miaka 8 ya uongozi wa kanisa. Wakati huohuo tayari makadinali wameshaanza kuwasili Roma kuanza kipindi cha kujadiliana kwa mujibu wa sheria za kanisa kuamua ni kina nani walio wagombea wenye nafasi nzuri ya kuchukua wadhifa huo wa papa. Askofu mkuu Robert Sarah mzaliwa wa Guinea, ambaye ni kadinali anayeongoza ofisi ya misaada ya Vatican  amewaambia waandishi wa habari kwamba viongozi wa kanisa watapaswa kumchagua papa mpya kwa utulivu na kuaminiana.

Mwandishi: Saumu mwasimba

Mhariri: Bruce Amani.