1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wayemeni wataka mabadiliko serikalini

27 Januari 2011

Wayemeni waliotiwa moyo na machafuko yaliyomngoa kiongozi wa Tunisia na kuenea hadi Misri,wameandamana kwa maelfu wakimtaka Rais Ali Abdullah Saleh aondoke madarakani,baada ya kutawala kwa zaidi ya miaka 30 nchini mwao.

https://p.dw.com/p/Qw5X
Photo Title:- Photo of a demonstration in one of the main streets in the capital Sana'a Photographer:- Fatima AL_Aghbari Photo taken in :-picture was taken in the capital Sanaa, 24.01.2011
Waandamanaji waliomiminika SanaaPicha: DW

Maandamano hayo yameitishwa na muungano wa vyama vya upinzani na yamefanywa sehemu nne mbali mbali katika mji mkuu Sanaa. Kiasi ya waandamanaji 10,000 walikusanyika kwenye Chuo Kikuu cha Sanaa na wengine wapatao kama 6,000 waliandamana sehemu nyingine. Polisi walikuwepo lakini hakuna mapambano yaliyoripotiwa. Waandamanaji hao wanadai hali bora ya maisha na mabadiliko ya kisiasa. Walikuwa na mabango na moja lilisema, "Tumechoshwa na hadaa; tumechoshwa na rushwa; tazameni pengo liliopo kati ya masikini na matajiri."

Hata chama tawala cha GPC, kiliandaa maandamano ya wafuasi wake samba samba na ya wapinzani. Mabango ya wafuasi wa serikali yalisema: "Hakuna kupindua demokrasia na katiba" Waziri wa mambo ya Ndani wa Yemen, Motahar Rashad al-Masri amekanusha kulinganisha maandamano ya Yemen na yale ya Tunisia yaliyomtimua kiongozi wa nchi hiyo Zine al-Abidine Ben Ali.

Mageuzi ya Katiba yapingwa na upinzani

Der jemenitische Staatspraesident Ali Abdallah Saleh am Donnerstag, 28. Februar 2008 im Schloss Bellevue in Berlin. (AP Photo/Fritz Re iss) Yemenite S
Rais wa Yemen, Ali Abdallah SalehPicha: AP

Rais Ali Abdullah Saleh ni mshirika mkuu wa Marekani katika vita dhidi ya waasi wa Kiyemeni walio wafuasi wa Al-Qaeda. Saleh alie madarakani tangu miongo kadhaa, alichaguliwa tena Septemba mwaka 2006 kwa awamu ya miaka saba. Ikiwa mswada wa kubadili katiba unaojadiliwa bungeni, licha ya kupingwa na vyama vya upinzani, utapitishwa basi hiyo itamruhusu Saleh kubakia madarakani kwa maisha.

Rais Saleh ameuhimiza upande wa upinzani kushiriki katika uchaguzi wa bunge uliopangwa kufanywa Aprili 27. Amesema, kutofanya hivyo ni kujiangamiza kisiasa. Vyama vya upinzani vimekataa kuunga mkono mageuzi ya katiba. Muda wa bunge la hivi sasa ulirefushwa kwa miaka miwili hadi mwezi wa Aprili kuambatana na makubaliano yaliyofikiwa Februari mwaka 2009, kati ya chama tawala GPC na vyama vya upinzani. Lengo ni kuwa na nafasi ya kujadili mageuzi ya kisiasa. Lakini mazungumzo hayo yamekwama na kamati maalum iliyoundwa kusimamia mageuzi imekutana mara moja tu. Saleh anatuhumiwa kutaka kumrithisha mwanae Ahmed ambae hivi sasa ni mkuu wa kikosi maalum cha ulinzi wa rais. Lakini hivi karibuni alikanusha tuhuma hizo.

Yemen inayopakana na Saudi Arabia, inakabiliwa na ukosefu mkubwa wa ajira, huku akiba yake ya mafuta na maji ikififia. Takriban nusu ya wakaazi wake milioni 23 wanaishi kwa kutumia dola 2 kwa siku au hata chini ya kiasi hicho na theluthi moja ya umma unateseka kwa njaa. Serikali pia inapambana na uasi, kusini mwa nchi, huku ikijaribu kuendeleza makubaliano ya kusitisha mapigano upande wa kaskazini. Wakati huo huo, inahangaika kulitokomeza kundi la waasi la al-Qaeda lililopiga kambi Yemen.

Mwandishi: P.Martin/AFPE/RTRE
Mpitiaji:Abdul-Rahman