1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wazalishaji mafuta washindwa kuafikiana Doha

18 Aprili 2016

Bei ya mafuta imeporomoka Jumatatu(18.04.2016) siku moja baada ya nchi kubwa zinazozalisha mafuta kushindwa kukubaliana katika mkutano muhimu wa shirika la nchi hizo OPEC huko Doha Qatar.

https://p.dw.com/p/1IXs5
Waziri wa nishati na viwanda wa Qatar Mohammed Saleh al-Sada akizungumza na waandishi habari
Waziri wa nishati na viwanda wa Qatar Mohammed Saleh al-Sada akizungumza na waandishi habariPicha: picture-alliance/dpa

Hatua hiyo imezusha wasiwasi mpya juu ya mahitaji ya usambazaji bidhaa hiyo katika soko la dunia.Mpango wa kusimamisha uzalishaji mafuta kwa nchi za OPEC na zile zisizo wanachama wa OPEC umekwama baada ya Saudi Arabia kulazimisha Iran ijiunge na mpango huo inaoupinga.

Licha ya kutolewa miito kuitaka Saudi Arabia kuyaokoa makubaliano hayo na kusaidia kuimarisha bei ya mafuta ghafi nchi hiyo imeonekana kuisakama Iran na kuilazimisha ijunge na mpango huo wa kuzuia uzalishaji wa mafuta kwa lengo la kulibana soko na hatimae kuimarisha bei ya bidhaa hiyo.Hata hivyo matukio yaliyotokana na mkutano wa Doha yanafufua hofu katika sekta ya mafuta kwamba nchi kubwa zinazozalisha bidhaa hiyo ziko katika mapambano kwa mara nyingine ya kuwania soko na hasa baada ya serikali ya mjini Riyadh kutishia kupandisha kwa kiwango cha juu uzalishajimafuta ikiwa mpango wa kusimamisha uzalishaji wa bidhaa hiyo hautafikiwa.

Waziri wa mafuta wa Iran Bijan Zangeneh katika mkutano uliopita wa OPEC mjini Vienna
Waziri wa mafuta wa Iran Bijan Zangeneh katika mkutano uliopita wa OPEC mjini ViennaPicha: Reuters/Bader

Baada ya mazungumzo ya muda mrefu yaliyoibua malumbano makali ya maneno kati ya wajumbe wa Saudi Arabia na Urusi wajumbe na mawaziri waliohudhuria mkutano huo walitangaza kwamba hakuna mwafaka uliofikiwa.Waziri wa nishati wa Qatar Mohammed al Sada aliwaambia waandishi habari kwamba muda zaidi unahitajika kwa pande zote kushauriana tena.

'Sote tunahitaji muda kwa ajili ya kushauriana na kutoka sasa hadi mkutano wa mwezi Juni wa Opec nchi zote wanachama zitashauriana na nchi nyingine.''

Saudi Arabia ambayo inaliongoza shirika hilo la OPEC imewaambia wajumbe kwamba inataka kuwaona wanachama wote wa jumuiya hiyo ya nchi zinazozalisha kwa wingi mafuta duniani kushiriki katika mpango huo wa kuzuia uzalishaji bidhaa hiyo ikiwemo Iran ambayo haikuhudhuria mazungumzo hayo ya Qatar.Iran imekataa kupunguza uzalishaji kwa lengo la kutaka kulidhibiti tena soko lake baada ya kuondolewa vikwazo na nchi za magharibi.Waziri wa mafuta wa Iran Bijan Zanganeh anasema mkutano huo wa Doha uliwahusu wale wanaotaka kusaini makubaliano hayo lakini sio wao.

''Hatuwezi kushirikiana na wao katika kusimamisha uzalishaji mafuta yetu wenyewe kwa maneno mengine kufanya hivyo inamaanisha tutakuwa tunajiwekea vikwazo wenyewe''

Kiasi nchi 18 zinazozalisha mafuta duniani ikiwemo zile zisikuwa wanachama wa OPEC kama Urusi zilikusanyika mjini Doha kwa kile kilichotarajiwa kuwa makubaliano yaliyokuwa yakitafutwa tangu mwezi Februari kwa lengo la kuimarisha bei ya mafuta kufikia Octoba mwaka huu.Hata hivyo duru zinasema ikiwa Iran itaridhia kushiriki mkutano huo Juni pili mazungumzo na wazalishaji mafuta nje ya OPEC yanaweza kuanza tena.Ikumbukwe kwamba Urusi ni mshirika mkubwa wa Iran na imekuwa ikiitetea haki ya Iran ya kutaka kuongeza uzalishaji wa mafuta baada ya kipindi cha vikwazo huku pia ikiiunga mkono jamhuri hiyo ya kiislamu katika mivutano yake mingi na Saudi Arabia.

Waziri wa Nishati wa Urusi akiwasili Doha
Waziri wa Nishati wa Urusi akiwasili DohaPicha: picture-alliance/dpa

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri:Josephat Charo