1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri atishia kutangaza hali ya hatari Ukraine

27 Januari 2014

Waziri wa Sheria wa Ukraine Olena Lukash ameonya kuwa anaweza kutangaza sheria ya hali ya hatari nchini humo, baada ya waandamanaji wenye msimamo mkali kuivamia na kuishikilia wizara yake mjini Kiev.

https://p.dw.com/p/1AxfP
Waandamanaji wakiwa mjini Kiev
Waandamanaji wakiwa mjini KievPicha: Reuters

Kauli hiyo ameitoa wakati kiongozi wa upinzani Vitali Klitschko amewataka waandamanaji kuondoka katika wizara hiyo. Olena Lukash anayeshiriki kwenye mazungumzo kati ya upinzani na Rais Viktor Yanukovych yenye lengo la kutafuta suluhisho la mzozo unaoendelea nchini Ukraine, amekiambia kituo cha televisheni cha nchi hiyo kwamba ataomba mazungumzo hayo yasitishwe, iwapo waandamanaji wataendelea kuishikilia wizara hiyo.

Amesema atalazimika kufanya hivyo iwapo waandamanaji hawataondoka mara moja kwenye jengo hilo na wajumbe wa mkutano huo hawatapewa nafasi ya kutafuta suluhisho la amani.

Lukash kuliomba baraza la usalama wa taifa

Aidha, Lukash amesema iwapo jengo hilo litaendelea kushikiliwa na waandamanaji, ataliomba baraza la usalama wa taifa kujadili kuhusu haja ya kutangaza sheria ya hali ya hatari nchini humo.

Maandamano yakiendelea Kiev
Maandamano yakiendelea KievPicha: Valeriy Lebid, Svitlana Dubyna, gre4ka.info

Hatua hiyo inatishia katika kutafuta suluhu ya mzozo wa kisiasa Ukraine, kabla ya kuanza kwa kikao maalum cha bunge, ambacho kiongozi wa upinzani, amekielezea kama ''Siku ya Hukumu.''

Waandamanaji wa kundi la Spilna Sprava, au ''Vitendo vya Ukweli'' waliingia kwenye jengo la wizara hiyo jana jioni na kuyavunja madirisha na kuharibu nembo ya wizara hiyo. Polisi wameanza uchunguzi kuhusu uhalifu uliofanyika katika uvamizi huo.

Katika juhudi za kuleta maridhiano na kumaliza mzozo huo nchini Ukraine, Rais Yanukovych amekubali kutoa ahadi mbalimbali kwa upinzani, kama vile kubadilisha katiba na kuwapa wapinzani nyadhifa kadhaa, ikiwemo nafasi ya waziri mkuu.

Yanukovych alipendekeza kumpa wadhfa wa waziri mkuu, kiongozi wa upinzani Arseniy Yatsenyuk na Klitschko awe naibu waziri mkuu anayehusika na masuala ya kibinaadamu. Hata hivyo, upinzani umesema ahadi hizo hazikidhi matakwa yao.

VIongozi wa Ulaya waisihi Ukraine

Viongozi wa Ulaya walitoa wito wa kufanyika kwa mazungumzo kati ya pande hizo mbili, wito uliosisitizwa pia na kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Baba Mtakatifu Francis, aliyetaka mzozo huo usitishwe na mahasimu waingie katika meza ya mazungumzo na kisha aliliombea taifa hilo katika sala maalum.

Rais Yanukovych akizungumza na viongozi wa upinzani
Rais Yanukovych akizungumza na viongozi wa upinzaniPicha: picture-alliance/dpa

Wakati huo huo, Klitschko, ambaye ni bingwa wa zamani wa ndondi amewataka waandamanaji kuondoka katika wizara hiyo.

Akizungumza kwenye mji mkuu wa Ukraine, Kiev, Klitschko amesema kuwa atajaribu kuwashawishi waandamanaji waondoke kwenye jengo la wizara hiyo, ingawa wanataka kubakia hapo.

Maandamano makubwa yalizuka katika mji mkuu wa Ukraine, Kiev mwaka uliopita, baada ya Rais Yanukovych kuamua kutosaini mkataba wa ushirikiano wa kibiashara na Umoja wa Ulaya na kuamua kuimarisha uhusiano wa nchi hiyo na Urusi.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFPE,DPAE
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman