1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ziara ya Pakistan.

Mtullya, Abdu Said28 Oktoba 2008

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank -Walter Steinmeier aitaka jumuiya ya kimataifa iisaidie Pakistan.

https://p.dw.com/p/Fj5o
Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier akisalimiana na rais Asif Ali Zardari wa Pakistan mjini Islamabad.Picha: picture-alliance/dpa

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani bwana Frank-Walter Steinmeier ametoa mwito kwa jumuiya ya kimataifa wa kuunga mkono juhudi za Pakistan katika kukabiliana na matatizo yaliyoifika nchi hiyo kutokana na mgogoro wa fedha.

Waziri Steinmeier ametoa mwito huo mjini Islamabad leo baada ya mazungumzo yake na rais Asif Ali Zardari wa Pakistan.

Waziri Frank-Walter Steinmeier amesema shirika la fedha la kimataifa IMF, linapaswa kutenga mkopo wa kutosha kwa ajili ya Pakistan ili kuiwezesha nchi hiyo kukabiliana na mgogoro wa fedha ulioikumba dunia nzima.

Waziri huyo wa Ujerumani amefanya ziara nchini Pakistan wakati ambapo nchi hiyo inakabiliwa na uhaba mkubwa wa fedha za kigeni na kiwango kikubwa cha mfumuko wa bei. Pakistan inakabiliwa na mgogoro wa uchumi huku akiba yake ya fedha za kigeni ikiendelea kukauka.Pakistan inakaribia kufilisika.Waziri Steinmeier amesema anatumai kwamba shirika la fedha la kimataifa IMF litachukua hatua za haraka ili kuisaidia Pakistan.

Katika ziara yake nchini Pakistan Waziri Steinmeier aliwahakikishia viongozi wa nchi hiyo kuwa Ujerumani itaongeza misaada yake kwa nchi hiyo hasa katika sekta za elimu na katika miradi ya nishati.

Pakistan inakabiliwa na mazingira ya hatari kubwa katika vita vyake dhidi ya magaidi wa al-kaida na taliban na vilevile katika sekta ya uchumi. Nchi hiyo inahitaji kiasi cha dola bilioni 4.5 ili kusawazisha nakisi katika urari wa malipo.

Waziri Frank-Walter Steinmeier pia alifanya mazungumzo na waziri mwenzake wa Pakistan bwana Shah Mehmood Qureshi.Waziri huyo ameutaka Umoja wa Ulaya ufungue soko lake kwa bidhaa za Pakistan na hasa ametaka kuondolewa kwa ushuru unaotozwa katika nguo.

Katika mazungumzo yake waziri Steinmeier pia alijadili suala la usalama ambapo ameilamu Marekani kwa mashambulio inayofanya kwenye maeneo ya mpaka baina ya Pakistan na Afghanistan.Waziri Steinmeier ameilaumu Marekani kwa kufanya mashambulio hayo bila ya kuijulisha serikali ya Pakistan. Amesema operesheni kama hizo hazina faida.

Waziri Frank Walter Steinmeier ameenda Saudi Arabia baada ya ziara yake nchini Pakistan.