1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri Mkuu al-Maliki aomba msaada Marekani

Abdu Said Mtullya1 Novemba 2013

Waziri Mkuu wa Irak Nuri al-Maliki anakutana na Rais Barack Obama mjini Washington wakati ambapo nchi yake inakabiliwa na wimbi kubwa la umwagikaji damu. Waziri Mkuu huyo ameenda Marekani kuomba msaada.

https://p.dw.com/p/1AANN
Waziri Muu wa Iraq Nuri al-Maliki
Waziri Mkuu wa Iraq Nuri al-MalikiPicha: picture-alliance/dpa/dpaweb

Rais Obama anasifika kwa kuvimaliza vita vya Iraq kwa kuyaondoa majeshi ya Marekani . Lakini Obama anakutana na mtu ambae bado anapigana vita hivyo-Waziri Mkuu Nuri al -Maliki.

Waziri Mkuu al-Maliki anakutana na Rais Obama wakati ambapo umwagikaji damu umefikia kiwango kisichokuwa na mithili nchini Iraq tokea mwaka 2008. Waziri Mkuu wa Iraq ameomba msaada wa Marekani ili aweze kukabiliana na hali hiyo miaka miwili baada ya majeshi ya Marekani kuondoka. Waziri Mkuu al- Maliki ameomba msaada wa zana zaidi za kijeshi sambamba na ushirikiano mkubwa zaidi katika mambo ya usalama baina ya nchi yake na Marekani .

Watu takriban 1000 wameuawa

Kwa mujibu wa taarifa ya wizara za afya, mambo ya ndani na ulinzi mwezi uliopita watu takriban 1000 waliuawa nchini Irak. Kati ya hao, 855 walikuwa raia,65 walikuwa polisi na wanajeshi 44. Watu wengine 1600 walijeruhiwa.Lakini taarifa ya Umoja wa Mataifa inaonyesha kwamba waliouawa ni wengi zaidi.

Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa Nickolay Mladenov amesema mauaji yanayofanyika kiholela yanaendelea mtindo mmoja. Waziri Mkuu wa Iraq ameifafanisha hali anayopambana nayo katika nchi yake inayotokana na mashambulio yanayofanywa na wapiganaji wenye uhusiano na Al-Qaeda na vita vikuu vya tatu.

Miaka miwili baada ya majeshi ya Marekani kuondoka Iraq nchi hiyo imesimama kwenye ukingo wa vita vingine vya kimadhehebu .Mauaji yameendelea leo(ijumaa) ambapo watu wanne waliuawa kaskazini mwa nchi hiyo.

Waziri Mkuu al-Maliki anatarajiwa kuiomba Marekani isaidie zaidi katika juhudi za kupambana na umwagijaki damu nchi mwake. Mwezi uliopita sehemu kadhaa za hadhara zilishambuliwa ikiwa pamoja na mikahawa, na bustani za mapimziko.Watu waliokuwa mazikoni pia waliwashambuliwa mara kwa.

Hata kwa Iraq mauaji yamezdi

Mtaalamu wa masuala ya Iraq kutoka Wakfu wa Ujerumani , Friedrich-Naumann ,Falko Walde amesema Iraq haijawahi kwua na utulivu tokea kuangushwa kwa Saddam Hussein.Ghasia zimetokea wakati wote lakini amesema hali ya sasa ni mbaya sana. Wizara ya mambo ya nje ya Marekani imesema watu wasiopungua 6,000 wameshaua mnamo mwaka huu nchini Iraq

Maafisa wa Ikulu ya Marekani wamesema Rais Obama atalijadili suala la usalama na Waziri Mkuu al-Maliki na kujaribu kutafuta njia za kupunguza umwagikaji wa damu nchini Iraq.

Mwandishi:Mtullya Abdu.afp,rtre

Mhariri: Yusuf Saumu