Waziri mkuu wa jimbo la Bavaria pia ang'atuka.
1 Oktoba 2008
Siku nne baada ya chama chake CSU kushindwa vibaya katika uchaguzi ,waziri mkuu wa jimbo la Bavaria Günther Beckstein leo ametangaza kujiuzulu.
Bwana Beckstein ameeleza kwamba baada ya chama chake kupoteza kura nyingi katika uchaguzi wa jimbo , sasa haoni kuwa anaungwa mkono na chama hicho, kwa kiasi cha kumwezesha kuunda serikali ya mseto.
Waziri mkuu Beckstein alifahamisha juu ya uamuzi wake wa kujiuzulu kwenye kikao maalumu cha chama chake mapema leo katika mji mkuu wa Bavaria, Munic baada ya wawakilishi wa mikoa kadhaa wa chama hicho kumtaka bwana Beckstein ang'atuke.
Bwana Beckstein ameeleza kuwa amejiuzulu kwa sababu chama chake hakimwuungi mkono baada ya kushindwa vibaya sana katika uchaguzi wa jumapili iliyopita.
Waziri mkuu huyo wa jimbo la Bavaria lililopo kusini mashariki mwa Ujerumani ameeleza kuwa itakuwa vigumu kutekeleza majukumu yake katika serikali ya mseto ya jimbo lake ikiwa haungwi mkono na chama chake kwa kiasi cha kutosha.
Kwa mujibu wa duru za ndani ya chama cha CSU,mwenyekiti mteule wa chama hicho bwana Horst Seehofer huenda akachukua wadhifa wa waziri mkuu vilevile ,wa jimbo hilo la Bavaria lenye nguvu kubwa za kiuchumi kuliko Sweden.
Lakini habari zaidi kutoka mji mkuu wa Bavaria Munic zinasema wanasiasa kadhaa wa chama cha CSU wanapinga wazo la bwana Seehofer ambae pia ni waziri wa kilimo na maslahi ya wateja katika serikali kuu, ya Ujerumani kuwa waziri mkuu wa Bavaria. Badala yake wanasiasa hao ikiwa pamoja na Spika wa bunge la Bavaria wanataka mtu mwengine awe waziri mkuu. Hatahivyo bwana Seehofer na waziri wa mambo ya ndani wa jimbo la Bavaria Joachim Herrmann kadhalika, wamesema kuwa wapo tayari ,kuziba pengo lililoachwa na bwana Günther Beckstein.Wanasiasa wengine wawili wa chama cha CSU pia wanawania nafasi hiyo.
Waziri mkuu wa jimbo la Rheinland -Palatinate bwana Kurt Beck amesema ni wazi kwamba bwana Beckstein amejizulu kutokana matokeo mabaya sana ya uchaguzi wa jumapili iliyopita katika jimbo la Bavaria.
Katika uchaguzi huo chama cha CSU kilipoteza viti zaidi ya 30 na hivyo kupoteza nafasi ya kuwa mtawala wa pekee katika jimbo la Bavaria kwa mara ya kwanza baada ya miaka 40. Kujiuzulu kwa bwana Beckstein kunafuatia kujiuzulu kwa mwenyekiti wa chama hicho cha CSU hapo jana Erwin huber.