1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hotuba ya Waziri Mkuu May yasubiriwa kwa hamu

Mohammed Abdulrahman
17 Januari 2017

Waziri mkuu  wa Uingereza Theresa May leo anatarajiwa kuelezea kwamba anaunga mkono utaratibu safi wa kujitoa kutoka Umoja wa Ulaya, na kuondoa uwezekano wa kujiondoa kwa sehemu tu katika mikataba  na Umoja huo.

https://p.dw.com/p/2VuL6
Belgien | EU-Gipfel | Theresa May
Picha: picture-alliance/Olivier Hoslet/EPA/dpa

Katika hotuba  inayosubiriwa kwa hamu, huenda Waziri mkuu May akaashiria kwamba Uingereza inaelekea katika kile ambacho wachambuzi wanakiita kuwa”hali ngumu ya kujitoa katika Umoja wa Ulaya. Bibi May atatoa hotuba yake kwenye jingo la Lancaster katikati mwa jiji la London, mahala ambapo ni kitovu cha shughuli za kidiplomasia na matangazo muhimu.

Kwa mujibu wa yaliomo ndani ya Hotuba hiyo iliotawanywa mapema kwa vyombo vya habari na makao makuu  ya  Waziri mkuu ya nambari kumi mtaa wa Downing, Bibi May anatarajiwa kueleza wazi kwamba , " hakuna kujitoa nusu , huku akisisitiza kwamba kujitoa yaani "Brexit " kunamaanisha kujitoa.

Hapana shaka muelekeo wake utashangiriwa na  waingereza wanaotaka  nchi yao ijitowe kutoka Umoja wa Ulaya na kuwavunja moyo mno wanaotaka ibakie kuwa mwanachama, ambao wanaofu kwamba kujiondoa kutrakuwa na athari kubwa kwa uchumi wa Uingereza.

England Demonstranten für und gegen den Brexit in London
Waandamanaji wanaopinga Uingereza kujiondoa Umoja wa Ulaya Picha: imago/Pacific Press Agency/A. Pezzali

Hotuba yake itagusia kila  pembe ya  mkakati wake wa kujitoa katika Umoja wa Ulaya wa wanachama 28 , baada ya miezi kadhaa ya taharuki na vuta nikuvute. Wadadisi walikwisha ashiria hivi karibuni kwamba Uingereza  itataka kujitoa kikamilifu, ili iweze kuwa na malaka ya kushughulikia kikamilifu  suala la wahamiaji. 

Hotuba ya Waziri mkuu May imetawala hii leo katika magazeti ya Uingereza, huku Daily Mail linalounga mkono  kujitoa, likionekana kusherehekea. Kichwa cha maneno cha toleo lake kinasema,” Uingereza huru na mpya ya Theresa May.” Hata hivyo  gazeti la Guardian linalopendelea Uingereza ibakie kuwa mwanachama wa Umoja wa Ulaya, limewaonya wanaopinga likisema watajuta.   

Sarafu ya Uingereza”Sterling” imeimarika kidogo leo baada ya kuteremka  thamani Jumatatu  katika hali  kiwango kisichowahi kushuhudiwa kwa miaka 31 iliopita. Pamoja na hayo waziri wa fedha Philip Hammond alisema anataka Uingereza iendelee kutambuliwa kuwa ina uchumi utakaofuata utaratibu wa Umoja wa Ulaya, ikiwa ni pamoja na  utaratibu wakodi na viwango sawa na Umoja huo.  Bibi May ameahidi kuanza  rasmi mazungumzo na Umoja wa Ulaya mwezi Machi na Mkuu wa Umoja huo anayehusika na  mazungumzo hayo Michel Barnier amesema makubaliano yanapaswa kufikiwa kabla ya uchaguzi wa bunge la Ulaya 2019.

London Britain's Prime Minister Theresa May greets her Polish counterpart Beata Szydlo in front of 10 Downing Street in central London
Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May akisalimiana na mwenzake wa Poland Beata Szydio mtaa wa DowningPicha: Reuters/P. Nicholls

Uingereza  itakayojitoa  kwenye Umoja huo, ni jambo lililopewa msukumo Jumapili na Rais mteule wa Marekani  Donald Trump ambaye alisema anaunga mkono kuwepo kwa  mkataba wa haraka wa kibiashara kati ya Marekani na Uingereza.  Lakini hata  ikiwa mpango wa Waziri mkuu wa Uingereza hii leo utapata uungaji mkono mkubwa nchini mwake, bado kuna changamoto za kisheria ambazo zinaweza kuucheklewesha mpango wa kujitoa.

Mahakama kuu ya Uingereza  inatarajiwa kuamua  baadae mwezi huu, iwapo Bibi May kwanza atahitaji  kibali cha bunge kabla ya kuanza mazungumzo ya kujitoa katika Umoja wa ulaya , jambo ambalo huenda likachelewesha  mazungumzo .

Mwandishi: Mohammed Abdul-Rahman / afp

Mhariri: Josephat Charo