1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri mkuu mpya wa China Li Keqiang ziarani India

20 Mei 2013

Waziri mkuu mpya wa china Li Keqiang ameichagua India kuwa kituo cha kwanza cha ziara yake nchi za nje na kuahidi kurejesha hali ya kuaminiana kati ya Beijing na New-Delhi.

https://p.dw.com/p/18avo
Waziri mkuu wa India Manmohan Singh(kushoto) na mgeni wake wa China Li KeqiangPicha: Reuters

Waziri mkuu mpya wa China amewasili tangu jana mjini New Delhi ambako alikuwa na mazungumzo ya siri pamoja na kiongozi mwenzake Manmohan Singh.Waziri mkuu wa India alilizusha suala la mivutano ya mpakani iliyosababisha damu kumwagika mnamo mwaka 1962.Viongozi hao wawili wamesisitiza umuhimu wa kuendelezwa amani na utulivu katika eneo hilo la mpakani.

Katika mkutano na waandishi habari waziri mkuu wa China amesema ameichagua India kuwa kituo cha kwanza cha ziara yake nchi za nje kwasababu ushirikiano kati ya madola haya mawili yenye wakaazi wengi zaidi duniani ni muhimu kwa utulivu wa dunia na kwa ukuaji wa kiuchumi.

Li Keqiang ameendelea kusema:"Kwa misingi ya hali ya kuaminiana,nchi zetu mbili zinaweza kuimarisha zaidi masikilizano ya pande mbili,kuanzisha uhusiano wa aina mpya kati ya madola mawili makuu na kuinua na kuendeleza uhusiano madhubuti kati ya China na India.Hiyo itakuwa neema ya kweli kwa Asia na ulimwengu kwa jumla."

Ziara ya waziri mkuu Li Keqiang nchini India imejiri wiki chache tu baada ya mvutano kuzidi makali katika eneo la mpaka unaozigawa nchi hizo mbili,wahindi wakiwatuhumu wachina kuingia April 15 iliyopita katika eneo la mlima Himalaya wanalodai kuwa ni milki yao.

Biashara ya pande mbili itaimarishwa

Li Keqiang Ministerpräsident China zu Besuch bei Manmohan Singh Premierminister Indien
Li Keqiang na Manmohan Singh wakiangalia sherehe za mapokezi katika uwanja wa kasri la rais Rashtrapati Bhavan mjini New-DelhiPicha: Reuters

Baada ya mazungumzo pamoja na waziri mkuu Manmohan Singh,waziri mkuu wa China amepangiwa kuzungumza pia na waziri wa mambo ya nchi za nje Salman Khurshid pamoja pia na viongozi wa chama kikuu cha upinzani-Bharatiya Janata-BJP.Kesho waziri mkuu wa China Li Keqiang atautembelea mji mkuu wa kiuchumi wa India Bombay.

China ni mshirika wa pili muhimu wa kibiashara wa India.Biashara kati ya nchi hizo mbili,kwa mujibu wa naibu waziri wa biashara wa China Jiang Yaoping imefikia dala bilioni 66.5 mwaka jana-Lengo lililowekwa ni kuhaakikisha ushirikiano wa kibiashara unafikia hadi dala bilioni 100 ifikapo mwaka 2015-amesema naibu waziri wa biashara wa China.

Mbali na India,waziri mkuu wa China Li Keqiang ataitembelea pia Pakistan,mshirika wa jadi wa China,Ujerumani na Uswisi ambako masuala ya kiuchumi yanatarajiwa kugubika mazungumzo.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir:AP/AFP/Reuters

Mhariri Mohammed Abdul-Rahman