1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri Mkuu wa Israel ziarani Ujerumani

27 Agosti 2009

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amewasili Berlin mji mkuu wa Ujerumani,Jumatano jioni kwa ziara ya siku mbili.

https://p.dw.com/p/JJK8
Bundespraesident Horst Koehler, rechts, begruesst den israelischen Ministerpraesidenten Benjamin Netanjahu, links, am Mittwoch, 26. August 2009, im Schloss Bellevue in Berlin. Netanyahu ist zu einem zweitaegigen Besuch in der deutschen Hauptstadt. (AP Photo/Franka Bruns) ---German President Horst Koehler, right, greets Israeli Prime Minister Benjamin Netanyahu, left, inside Bellevue Castle in Berlin, Wednesday, Aug. 26, 2009. Netanyahu is in German for a two-day visit. (AP Photo/Franka Bruns)
Rais wa Ujerumani Horst Köhler(kulia) akimkaribisha Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu.Picha: AP

Hii ni ziara yake kwanza nchini Ujerumani tangu kiongozi huyo wa chama cha kihafidhina Likud kuchaguliwa kuiongoza serikali ya Israel katika mwezi wa Machi. Mchakato wa amani katika Mashariki ya Kati ni mada itakayopewa kipaumbele wakati wa majadiliano ya Netanyahu na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel baadae leo hii.

Waziri Mkuu Netanyahu jana jioni alikutana na Rais wa Ujerumani Horst Köhler baada ya kuwasili kutoka London ambako alikuwa na majadiliano pamoja na mjumbe maalum wa Marekani katika Mashariki ya Kati George Mitchell.Leo asubuhi amekutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier na baadae atakuwa na majadiliano pamoja na Kansela Angela Merkel na mada kuu ni mchakato wa amani katika Mashariki ya Kati.

Kabla ya ziara ya Netanyahu,Merkel mara nyingine tena alitoa wito wa kutekelezwa suluhisho la mataifa mawili. Amesema, nafasi iliyopo hivi sasa isiachiliwe kupotea.Katika mahojiano yake na kituo cha televisheni cha Ujerumani N24 Merkel alisema mazungumzo ya amani kati ya Israel na Wapalestina yanapaswa kuanzishwa tena. Baada ya rais mpya wa Marekani Barack Obama kuingia madarakani,uwezekano wa kupata suluhisho la mataifa mawili umeongezeka na huu ni wakati ulio sahihi kabisa na kila juhudi ifanywe kuitumia nafasi hiyo aliongezea Kansela wa Ujerumani.

Lakini siku ya Jumatano redio ya Israel iliarifu kuwa Waziri Mkuu Netanyahu hatoitikia wito wa Rais Obama kusitisha kabisa ujenzi wa makazi ya walowezi wa Kiyahudi katika ardhi iliyozikalia.Netanyahu atapinga kabisa kusitisha ujenzi katika Jerusalem ya Mashariki.

Lakini siku za karibuni, uvumi umekuwa ukienea kuwa Israel na serikali ya Obama zinakaribia kuafikiana.Vyombo vya habari vinaripoti kuwa Waisraeli wapo tayari kusitisha ujenzi kwa muda wa hadi mwaka mmoja katika Ukingo wa Magharibi. Wakati huo huo, gazeti la Israel Haaretz limeripoti kuwa kabla ya Netanyahu kuanza ziara yake, Kansela wa Ujerumani alishinikizwa kutolizusha suala la makazi ya walowezi wakati wa mkutano wao hasa watakapokuwa na mkutano wa pamoja na waandishi wa habari.Ombi hilo limekataliwa na mshauri wa masuala ya nje na sera za usalama wa Kansela Merkel.

Mwandishi:C.Verenkotte/ZPR/P.Martin/DPA

Mhariri: M.Abdul-Rahman