1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Thobane alitakiwa kufika mahakamani Ijumaa

Ibrahim Swaibu
21 Februari 2020

Waziri mkuu wa Lesotho Thomas Thabane ameshindwa kufika mahakamani Ijumaa kujibu mashtaka ya mauaji ya  aliyekuwa mke wake, Lilopelo Thabane.

https://p.dw.com/p/3Y8YU
Thomas Motsoahae Thabane Premierminister Lesotho
Picha: picture-alliance/dpa

Waziri mkuu wa Lesotho Thabane ameshindwa kufika mahakamani Ijumaa kujibu mashtaka ya mauaji ya  aliyekuwa mke wake, Lilopelo Thabane 58. Waziri huyo alitakiwa kufika mahakamani leo hii lakini katibu wake Thabo Thakalekoala amewaambia wandishi wa habari kuwa Thomas mwenye umri wa miaka 80 amesafiri kwenda Afrika Kusini kufanyiwa uchunguzi wa afya yake na hataweza kufika mahakamani.

Soma zaidi: Lesotho: Chama cha Waziri Mkuu chamtaka ajiuzulu

Mnamo siku ya Alhamisi naibu kamishna wa polisi nchini humo Paseka Mokete alisema kuwa waziri Thabane atafikishwa mahakamani Ijumaa kwa mashtaka ya mauaji ya aliyekuwa mke wake, Lilopelo Thabane.

Lilopelo, aliuawa nyumbani kwake kwa kupigwa risasi mnano mwaka 2017 katika mji mkuu Maseru, siku mbili kabla ya kuapishwa kwa Thomas Thabane kama waziri mkuu wa  Lesotho.

Mauaji yalitikisa nchi

Mauaji ya Bi Lilopelo ambayo yalitokea wakati wanadoa hao walipokuwa wakivutana kuhusu talaka yaliitikisa nchi hiyo ndogo ya kusini mwa Afrika.

Lesotho Prozess Premierminister Thomas Thabane
Waziri Thomas Thabane hakuonekana kizimbani Picha: Reuters/Sumaya Hisham

Waziri kisha alimuoa Bi Maesaiah Thabane, ambaye kwa sasa ni mama wa kwanza wa taifa hilo, naye pia anakabiliwa na kesi ya mauaji ya Lilopelo. Atafikishwa tena mahakamani Machi 17.

Shirika la habari la AFP limeripoti kuwa Thabane aliondoka Lesotho Alhamsi siku ambayo polisi ilisema atafikishwa mahakamani kusomewa mashitaka ya kesi hiyo.

Mapema Ijumaa, waziri huyo ametangaza kupitia runinga ya taifa kuwa atajiuzulu mwishoni mwa mwezi Julai kutokana na umri wake mkubwa.

''Hajakimbia kutoka nchini, ameenda kwa daktari Afrika Kusini," mwanawe waziri, Potlako Thabane ameliambia shirika la habari la Reuters kwa njia ya simu.

Chanzo: AFPE