1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri mkuu wa New Zealand ausifu mkutano wa Commonwealth

26 Novemba 2007
https://p.dw.com/p/CT3B

Waziri mkuu wa New Zealand, Helen Clark, amesema leo kwamba mkutano wa jumuiya ya madola, Commonwealth, uliomalizika jana mjini Kampala Uganda, umefaulu kupiga hatua katika juhudi za kimataifa za kupunguza ongezeko la joto duniani.

Katika taarifa yake, Helen Clark, aliyehudhuria mkutano huo wa kilele uliozileta pamoja nchi 53 wanachama wa jumuiya ya madola, amesema tangazo la pamoja la mkutano wa mjini Kampala kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa limetoa mchango mkubwa katika kukabiliana na utoaji wa gesi chafu za viwandani.

Tangazo hilo hata hivyo halina mafungamano kuhusu kujitolea kuyalinda mazingira.

Clark ameongeza kusema mkutano wa Commonwelath ni wa tatu wa kimataifa katika miezi mitatu iliyopita, kuwa na ajenda kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa kama mada kuu ya mkutano.

Mkutano wa kikanda kati ya Asia na Pacific uliofanyika mjini Sydney, Australia, mkutano wa nchi za Asia Mashariki na hatimaye mkutano wa Commonwelath, yote inaendeleza kasi kufikia mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa utakaofanyika kisiwani Bali nchini Indonesia mwezi ujao.