1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri Mkuu wa Thailand aijuzulu

Halima Nyanza4 Julai 2011

Waziri Mkuu wa Thailand anayemaliza muda wake, Abhisit Vejjajiva, amejiuzulu hii leo (04.07.2011), kuongoza chama chake cha Democrat, baada ya kushindwa vibaya na chama cha upinzani katika uchaguzi uliofanyika jana.

https://p.dw.com/p/11oQS
Waziri Mkuu Abhisit Vejjajiva na familia yake kabla ya kushindwa
Waziri Mkuu Abhisit Vejjajiva na familia yake kabla ya kushindwaPicha: AP

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Bangkok mara baada ya kutangazwa matokeo, Vejjajiva amesema kama kiongozi wa chama cha Democrat, anakiri kuwa safari hii wameshinda viti vichache kuliko ilivyokuwa katika uchaguzi uliopita wa mwaka 2007, hivyo kama kiongozi bora anapaswa kuwajibika kwa kujiuzulu.

Abhisit ameyakubali pia matokeo ya uchaguzi huo na kukiri kushindwa kwa chama chake. Na hakusita kuwapongeza wapinza kwa ushindi waliopata.

Aidha amefahamisha kuwa chama chake kitafanya mkutano wake mkuu katika muda wa siku 90, kuchagua kiongozi mpya.

Naye, Waziri wa Ulinzi anayemaliza muda wake na aliyekuwa mkuu wa majeshi wa nchi hiyo, Prawit Wongsuwan, amesema leo kwamba jeshi la nchi hiyo limeukubali ushindi waliopata wapinzani katika uchaguzi huo, na kwamba halitawazuia kuunda serikali.

Tume ya uchaguzi nchini humo imesema chama cha Democrat kimepata viti 159 kati ya viti 500 katika bunge la nchi hiyo. Huku chama cha upinzani cha Puea Thai kikiibuka na viti 265.

Thida Tojirakarn Red Shirts Thailand
WapinzaniPicha: AP

Matokeo hayo yanatoa njia, kwa dada wa aliyewahi kuwa Waziri mkuu wa nchi hiyo Thaksin Shinawatra, Yingluck Shinawatra kuwa Waziri mkuu wa kwanza mwanamke nchini humo.

Lakini hata hivyo chama chake kitaunda serikali ya pamoja na chama kingine kidogo cha Chatthaipattana ambacho kimepata viti 19. Huku chama kingine cha Chatpattana Pheupandin kikitarajia pia kujiunga, kuunda serikali.

Yingluck Shinawatra, aliyewahi kuwa mfanyabiashara na ambaye hana uzoefu mkubwa wa masuala ya siasa, anaelekea kushika wadhfa huo, baada ya kaka yake Thaksin Shinawatra, ambaye bado ni maarufu nchini humo licha ya kupinduliwa madaraka mwaka 2006 na ambaye ni kiongozi asiyepingwa wa chama hicho cha Pheu Thai, kumchagua dada yake huyo kama mgombea wa nafasi ya Uwaziri mkuu.

Hata hivyo, akizungumzia sababu zilizomfanya kushinda, amesema si kutokana na kubebwa na jina lake.

Akizungumzia ushindi huo, mfanya biashara na bilionea wa zamani Thaksin Shinawatra ambaye amekuwa akiishi uhamishoni toka mwaka 2008, kuepuka kifungo cha miaka miwili gerezani, baada ya kupatikana na hatia ya kutumia madaraka vibaya, amesema dada yake anakabiliwa na kazi kubwa katika siku za baadaye.

Aidha wachambuzi wamasema kwamba juhudi zozote zitakazofanywa na chama cha Pheu Thai, kutoa msamaha kwa kiongozi huyo wa zamani anayekabiliwa na tuhuma za rushwa kutasababisha upinzani mkubwa nchini humo.

Mwandishi: Halima Nyanza(dap,afp)

Mhariri:Yusuf Saumu