1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri mkuu wa Uengereza, Tony Blair, awasili kwa ghafla mjini Baghdad.

17 Desemba 2006
https://p.dw.com/p/CBHv

Baghdad:

Waziri mkuu wa Uengereza, Tony Blair, ameyataka mataifa ya dunia yamuunge mkono waziri mkuu wa Iraq, Nuri al-Maliki, ambaye yuko katika shida. Alipofika Baghdad kwa ghafla, Tony Blair hasa alizipongeza juhudi za al-Maliki za kutaka kuweko masikilizano baina ya makundi yanayopigana katika Iraq. Alisisitiza kwamba, kimsingi, mkakati wa Uengereza kuelekea Iraq hautabadilika. Pomoja na al-Maliki alikariri mwito wake kwamba madaraka ya kivita katika mikoa yakabidhiwe zaidi kwa wanajeshi wa Iraq.

Tony Blair amesimama huko Baghdad akiwa ziarani katika eneo la Mashariki ya Kati. Ameshazuri Misri na Uturuki.

Jana waziri mkuu wa Iraq, Nuri al-Maliki alitangaza kwamba maafisa wa kijeshi wa zamani katika wakati wa utawala wa Saadam Hussein wataingizwa katika jeshi na wanachama wa Chama cha Baath cha mdikteta huyo wa zamani pindi wanataka wataingizwa katika maisha ya utumishi wa serekali.

Wakati huo huo, watu waliokuwa na bunduki wakivaa sare za jeshi waliwateka nyara hadi wafanya kazi 30 wa ofisi ya Baghdad ya Shirika la Mwezi Mchanga la Iraq. Polisi ilisema watu hao waliokuwa na bunduki waliwasili hapo na magari na wakawachukuwa wafanya kazi, wakiwaacha wanawake. Shirika hilo la Mwezi Mchanga, ambalo ni sehemu ya Shirika la Msalaba Mwekundu Duniani, lina wafanya kazi 1000 huko Iraq.

Na kwa upande mwengine, bomu lililotegwa bembeni mwa barabara limewauwa wanajeshi watatu wa Kimarekani na kumjeruhi mwengine mmoja kaskazini ya mji mkuu wa Baghdad. Idadi hiyo inafanya kuwa zaidi ya 60 wanajeshi wa Kimarekani waliouliwa huko Iraq mwezi huu wa Disemba. Licha ya hayo, si chini ya Wa-Iraqi 23 waliuliwa jana, wakiwemo shehe na mwanasiasa wa madhehebu ya Sunni ambao walifyetuliwa risasi huko Iskandariya, kusini mwa Baghdad.