1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri mkuu wa Uengereza ziarani Afghanistan na Pakistan

Oumilkher Hamidou27 Aprili 2009

Uengereza yajiandaa kutia njiani mkakati mpya dhidi ya magaidi

https://p.dw.com/p/HfIX
Waziri mkuu wa Uengereza Gordon BrownPicha: AP

Waziri mkuu wa Uengereza Gordon Brown amewasili Islamabad hivi punde baada ya ziara ya ghafla nchini Afghanistan ambako alizungumza na rais Hamid Karzai kuhusu mkakati mpya wa kupambana na"maficho ya magaidi" nchini Afghanistan na Pakistan.

Waziri mkuu wa Uengereza amesema mkakati huo mpya wa nchi yake unazihusu Afghanistan na Pakistan pia.

"Maeneo ya mpakani kati ya Pakistan na Afghanistan yamegeuka " maficho na bustani ya magaidi".

"Njia ya maovu inayounganisha maeneo hayo na njia kadhaa zinazoelekea katika miji mikuu ya ulimwengu mzima" amesema hayo waziri mkuu wa Uengereza wakati wa mkutano na waandishi habari ,mwishoni mwa mazungumzo yake pamoja na rais Hamid Karsai wa Afghanistan.

Akizungumzia juu ya uchaguzi wa rais Agosti 20 ijayo,ambapo rais Hamid Karzai ameshatangaza atatetea wadhifa wake,waziri mkuu huyo wa Uengereza amesema tunamnukuu:

"Mwaka huu wa uchaguzi ni kipimo kwetu sote,lakini chaguo ni bayana:kupambana na nadharia kali nchini Pakistan au nchini Afghanistan au tuwaachie watuingilie" .Mwisho wa kumnukuu waziri mkuu Gordon Brown.

Mkakati huo mpya unatazamiwa kufafanuliwa,waziri mkuu huyo atakapolihutubia bunge la nchi yake jumatano ijayo mjini London.

Mkakati mpya wa Uengereza unazungumziwa katika wakati ambapo jeshi la Pakistan limeanza kujibisha hujuma za wataliban katika maeneo ya kaskazini magharibi ambako wataliban wanazidi kusonga mbele na mapambano yanazidi kupamba moto pia nchini Afghanistan.

Waziri mkuu wa Uengereza ameanza safari yake nchini Afghanistan kwa kuwatembelea wanajeshi wa nchi yake katika kambi ya Lashkar Gah katika jimbo la kusini la Helmand-ngome ya wataliban na kituo kimoja wapo kikubwa yanakooteshwa madawa ya kulevya.

Mwishoni mwa mazungumzo pamoja na rais Hamid Karzai mjini Kaboul,waziri mkuu huyo wa Uengereza ameelekea Pakistan kwa mazungumzo pamoja na rais Asif Ali Zardai.

Mara baada ya kuwasili mjini Islamabad waziri mkuu wa Uengereza amewahakikishia wananchi wa Pakistan na Uengereza kua licha ya kitisho cha wataliban wamedhamiria kwa pamoja kuzidisha juhudi zao katika kutia njiani hatua mpya na kufungua uhusiano wa aina mpya kati ya nchi zao mbili.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir

Mhariri:Abdul Rahman