1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Brown na Obama wakutana.

Abdu Said Mtullya4 Machi 2009

Waziri Mkuu wa Uingereza Gordon Brown asisitiza umuhimu wa mpango wa pamoja katika kuukabili mgogoro wa uchumi duniani.

https://p.dw.com/p/H5Mu
Rais Barack Obama na mgeni wake Waziri Mkuu wa Uingereza Gordon Brown.Picha: AP

Waziri Mkuu wa Uingereza Gordon Brown  anaendelea na ziara  ya nchini Marekani   amekutana na rais Barack Obama mjini  Washington  leo anatarajiwa  kulihutubia  bunge la nchi hiyo.

Waziri Mkuu Brown na mwenyeji wake rais Obama wamejadili  haja ya kuratibisha juhudi zao katika kukabiliana na mgogoro wa uchumi ulioikumba dunia.

Waziri mkuu Brown ametoa mwito juu ya kuwapo mpango mpya wa kimataifa kama ule uliotekelezwa na Marekani katika kukabiliana  na msambaratiko wa uchumi ulioikumba  dunia mnamo miaka 1930.

Amesema katika miezi ijayo patakuwa na uwezekano wa kuanzisha mpango huo mpya  wa kuzijumuisha nchi zote, kwa lengo la kurekebisha mfumo wa mabenki duniani.

Bwana Brown ambae ni kiongozi wa kwanza   wa Ulaya kukutana na rais Obama kwenye Ikulu ya Marekani anatumai kuungwa mkono  na Marekani katika dhamira ya kuanzisha udhibiti mkali katika mfumo  wa mabenki wa kimataifa.

Kwenye mazungumzo yao viongozi hao wa Uingereza na Marekani pia walijadili mkutano wa nchi tajiri na zinazoinukia kiuchumi za G- 20 utakaofanyika mjini London mwezi ujao.Viongozi hao pia wamejadili hali ya  Afghanistan inayozidi kuzorota.

Waziri Mkuu Brown leo anatarajiwa kuyahutubia mabaraza yote mawili ya bunge la Marekani ambapo anatazamiwa kutoa  mwito juu ya kusaidia katika juhudi za kuondoa vurumai iliopo katika mfumo  wa mabenki.

Bwana Brown pia atatoa mwito juu ya kupinga sera  za kujenga vizingiti katika uhusiano wa biashara na uchumi.