1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri Mkuu wa zamani wa Israel apewa miezi 8 jela

25 Mei 2015

Aliyekuwa waziri mkuu wa Israel Ehud Olmert amehukumiwa kwenda jela miezi minane baada ya kupatikana na hatia ya ufisadi. Tayari wakili wa mwanasiasa huyo amesema watakataa rufaa dhidi ya hukumu hiyo.

https://p.dw.com/p/1FW4d
Waziri Mkuu wa Zamani wa Israel, Ehud Olmert akiingia mahakamani
Waziri Mkuu wa Zamani wa Israel, Ehud Olmert akiingia mahakamaniPicha: picture-alliance/AP/F. O'Reilly

Hukumu hiyo iliyotolewa leo Jumatatu ni pigo jipya kwa bwana Ehud Olmert mwenye umri wa miaka 69, kwani tayari anakabiliwa na hukumu nyingine ya kifungo cha miaka sita, ambayo ilitolewa dhidi yake katika kesi nyingine ya ulaji rushwa, ambayo imekatiwa rufaa katika mahakama kuu.

Hukumu hiyo ilitolewa na mahakama ya mjini Jerusalem mwezi Machi, baada ya kusikilizwa tena kwa kesi dhidi ya Olmert, ambapo anatuhumiwa kupokea bahasha iliyojaa fedha kutoka kwa mfanyabiashara wa kimarekani, wakati alipokuwa waziri wa biashara mnamo miaka ya 2000.

Uvunjaji wa uaminifu

Majaji watatu waliopitisha hukumu ya leo, wamesema kwamba mwenendo wa Ehud Olmert unastahili adhabu ya kifungo gerezani. 'Mtumishi wa umma, waziri, ambaye anapokea dola za rushwa, na kuzitunza katika kabati la siri, na kisha akazitumia kwa maslahi yake binafsi, anafanya uhalifu, ambao unaondoa imani ya wananchi katika ofisi ya umma'. Wamesema majaji hao.

Olmert anatuhumiwa kupokea 'bahasha' kutoka mwekezaji aliyejenga nyumba hizi.
Olmert anatuhumiwa kupokea 'bahasha' kutoka mwekezaji aliyejenga nyumba hizi.Picha: MENAHEM KAHANA/AFP/Getty Images

Hali kadhalika, majaji hao wamempa Ehud Olmert kifungo cha ziada cha miezi minane ambacho atakitumikia akiwa nje, na faini ya kiasi cha dola 25,000. Wamesema adhabu hiyo kwa waziri mkuu wa zamani ni ndogo, kwa sababu wanatambua mchango wake kwa taifa. Mwendesha mashtaka wa nchi, Uri Korev amezungumzia adhabu hiyo aliyopewa Ehud Olmert.

''Mahakama imetuma ujumbe unaoeleweka leo, ujumbe unaosikika vyema, ambao kwao bendera nyeusi inapepea juu ya matendo maovu ya mtuhumiwa. Mahakama imeamua kwamba hakuna adhambu nyingine inayofaa ispokuwa kifungo jela, na kama tulivyoomba, amepewa adhabu ya kwenda jela'' Amesema mwendeshamashitaka huyo.

Udhalilishaji wa kikatili

Ehud Olmert ambaye alikuwa waziri mkuu wa Israel kati ya mwaka 2006 na 2009 amekuwa akishikilia kwamba hana hatia, na kuitaja kesi dhidi yake kuwa udhalilishaji wa kikatili.

Ehud Olmert ndiye waziri mkuu wa zamani wa Israel wa kwanza kufungwa kwa hatia ya kupokea rushwa
Ehud Olmert ndiye waziri mkuu wa zamani wa Israel wa kwanza kufungwa kwa hatia ya kupokea rushwaPicha: Reuters

Mnamo mwaka 2012 bwana Olmert alikuwa amefutiwa mashitaka ya ufisadi na magendo, na kutozwa tu faini ya dola 19,000 pamoja na kifungo cha nje kwa hatia ya kuvunja uaminifu. Hata hivyo ushahidi mpya iliibuka katika kesi nyingine dhidi yake, hali iliyowafanya waendesha mashitaka kurejelea kesi ya awali.

Kifungo cha miaka sita alichopewa Olmert mwezi Mei mwaka jana kilikuwa cha kwanza kinachohusiana na ufisadi dhidi ya mtu aliyewahi kuwa waziri mkuu wa Israel. Kilitolewa baada ya kesi iliyoendeshwa kwa miaka miwili, akituhumiwa kupokea rushwa ya Shekel 560,000, hiyo ikiwa sarafu itumiwayo nchini Israel, wakati alipokuwa meya wa mji wa Jerusalem kati ya mwaka 1993 na 2003, kutoka kwa mwekezaji aliyetaka kujenga nyumba za makazi ya watu katika mji huo.

Ehud Olmert alijiuzulu wadhifa wa waziri mkuu Septemba mwaka 2008, baada ya agizo la polisi kwamba alifaa kufunguliwa mashitaka, lakini aliendelea kushikilia ofisi hiyo hadi alipochaguliwa waziri mkuu wa sasa wa Israel Benjamin Netanyahu.

Mwandishi: Daniel Gakuba/rtre/afpe/dpae

Mhariri:Yusuf Saumu