1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Steinmeier asema hali ni tete

29 Mei 2015

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank- Walter Steinmeier amesema Urusi ndiyo iliyousababisha mgogoro wa nchini Ukraine kutokana na sera yake ya mvutano Steinmeier aliyasema hayo baada kuwasili nchini Ukraine_

https://p.dw.com/p/1FZAu
Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Steinmeier
Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani SteinmeierPicha: picture-alliance/dpa/J. Büttner

Waziri Steinemeier ameeleza kwamba mgogoro wa mashariki mwa Ukraine umetokana na sera ya ushari ya Urusi. Shirika la habari la Urusi Interfax limemnukulu Waziri huyo wa Ujerumani akisema kwamba hatua ya Urusi ya kuliteka jimbo la Crimea na hatua zake za kijeshi mashariki mwa Ukraine ni ushahidi wa sera ya mvutano inayotekelezwa na Urusi.

Bwana Steinmeier amesisitiza kwamba vikwazo vilivyowekwa na serikali za magharibi dhidi ya Urusi vitaondolewa ikiwa makubaliano ya kusimamisha mapigano yatatekelezwa kikamilifu.

Mkataba lazima utekelezwe kikamilifu

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani amesema nchi za magharibi zimewasilisha ujumbe wazi kabisa kwa Urusi: vikwazo vilivyowekwa na jumuiya ya kimataifa dhidi ya Urusi vinahusiana moja kwa moja na kutekelezwa kwa makubaliano yaliyofikiwa.

Makubaliano juu ya kusimamisha mapigano mashariki mwa Ukraine ambayo ni pili tangu mwezi wa Septemba yalitiwa saini na viongozi wa Urusi, Ukraine,Ufaransa,Ujerumani na Ufaransa kwenye mkutano uliofanyika katika mji mkuu wa Belarus, Minsk mnamo mwezi wa Februari.

Lakini makubaliano hayo yamekiukwa mara kadhaa na pande zote mbili-Ukraine na waasi wanaotaka kujitenga mashariki mwa nchi hiyo. Taarifa hiyo imetolewa na Shirika la Usalama na Ushirikiano barani Ulaya, OSCE.

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Steinmeier amezitaka pande zote ziyazingatie makubaliano ya kusimamisha mapigano kwa sababu mgogoro wa Ukraine hauwezi kutatuliwa kwa njia ya nguvu za kijeshi.

Hapo kesho Waziri huyo atakwenda katika mji wa Dnipropetrovsk ambao ni wa nne kwa ukubwa nchini Ukraine. Hii ni mara ya kwanza kwa Waziri Steinmeier kufanya ziara nchini Ukraine mnamo mwaka huu.

Ukraine yalemewa na deni

Waziri huyo anafanya ziara nchini Ukraine wakati ambapo nchi hiyo pia inakabiliwa na hatari ya kufilisika. Waziri wa fedha wa Ukraine Natalie Jaresko amesema kwamba nchi yake inafanya mazungumzo na wadai binafsi juu ya kuubadilisha utaratibu wa malipo ili kuiepesha Ukraine kushindwa kuyalipa madeni yake.

Wakati nchi hiyo imelemewa na mzigo wa deni, mfumuko wa bei ulifikia asilimia 60.9 mwezi uliopita. Na pana uwezekano mkubwa wa kiwango hicho kuongezeka. Uzalishaji viwandani umeanguka kwa asilimia 23 zaidi.

Wakati huo huo Ukraine inapaswa kulipa deni la Euro Bilioni 3 kwa Urusi hadi mwishoni mwa mwaka huu la sivyo Urusi inaweza kuipeleka Ukraine kwenye mahakama ya kimataifa. Na mahakama hiyo inaweza kuamua kwamba nchi hiyo haina uwezo wa kuyalipa madeni yake.

Mwandishi:Mtullya Abdu./afpe.

Mhariri:Yusuf Saumu