1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri Steinmeier wa Ujerumani ashtakiwa

Maja Dreyer24 Januari 2007

Kesi ya Mjerumani wa asili ya Kituruki, Murat Kurnaz, ambaye alifungwa katika gereza la Guantanamo na sasa kuishtaki serikali ya Ujerumani kwa kuchelewa kumrejesha nyumbani, hilo ndilo suala moja katika udondozi wa magazeti ya Ujerumani hii leo. Jingine ni kesi dhidi ya rais Katzav wa Israeli anayeshtakiwa kwa madai ya ubakaji.

https://p.dw.com/p/CHTu

Kwa mara ya kwanza, waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani, Franz-Walter Steinmeier, alijitetea dhidi ya madai ya kwamba alikataa kumsaidia mfungwa huyu wa Kijerumani Murat Kunraz kumrejesha kutoka kambi ya Guatanamo. Kamati ya bunge la Umoja wa Ulaya inayoshughulikia masuala yanayohusiana na idara za ujasusi za Marekani CIA pamoja na Kurnaz mwenyewe walimlaumu waziri Steinmeier kwa kumchelewesha mfungwa huyu kurudi nyumbani. Haya ni maoni yaliyoandikwa katika gazeti la “Allgemeine Zeitung” la mjini Mainz:
“Baada ya Steinmeier kukanusha shtaka hilo dhidi yake, basi ni maneno yake dhidi ya yale ya wabunge wa Ulaya na wakili wa Bw. Kurnaz. Afadhali Steinmeier awe na uhakika kamili kwamba hana hatia ili asianguke.”

Kwa maoni ya gazeti la “Pforzheimer Zeitung” kesi hiyo inaiathiri sana serikali iliyopita ya Ujerumani. Limeandika:
“Bw. Kurnaz alifungwa katika jela la Marekani la Guantanamo kwa miaka kadhaa bila ya kuwa na hatia. Hivyo serikali ya zamani ambayo ilitetea sana haki za kibinadamu ziheshimiwe katika nchi nyingine, lakini yenyewe ilivunja haki hizo. Lazima sasa iwekwe wazi, serikali ilikuwa na jukumu gani katika kesi hiyo?”

Na hatimaye kuhusu suala hili ni gazeti la “Neue Ruhrzeitung” la kutoka Essen ambalo limeandika yafuatayo:
“Serikali ya Ujerumani ingeweza kufunga kesi hiyo mapema. Lakini badala ya kumrejesha nyumbani mfungwa huyu, serikali haijachukua hatua yoyote na hata kuzuia Kurnaz kurudi nchini humu. Vyovyote vile, ikiwa mfungwa huyu angekuwa ni Mjerumani wa asili ya Kijerumani mwenye pasipoti ya Kijerumani, bila shaka kesi hiyo haingetokea.”

Na sasa tunaelekea Israel ambapo rais Mosche Katzav anashtakiwa kwa madai ya ubakaji. Haya hapa ni maoni yaliyoandikwa na mhariri wa gazeti la “Kieler Nachrichten ambaye anasema:

“Demokrasi ya Israel inaingia katika hatari. Rais anashtakiwa kwa madai ya ubakaji. Waziri mkuu anatuhumiwa kula rushwa. Na vyama vikubwa vya serikali havina havina nguvu tena. Ili kuzuia wanasiasa wa msimamo mkali kujipatia uungwaji mkono, lazima rais Katzav na waziri mkuu Olmert wajiuzulu. Hiyo ni hatua ya kwanza ya kujinusuru. Hadi sasa lakini inaonekana kama itabidi wanasiasa hawa wafukuzwe kutoka vyeo vyao. Basi hii inalingana na siasa za Libanon.”