1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier azuru China.

Kitojo, Sekione13 Juni 2008

Uhusiano baina ya China na Ujerumani sasa warejea katika hali bora.

https://p.dw.com/p/EJK0
Waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier baada ya mazungumzo na waziri mkuu wa China Wen Jiabao leo Ijumaa.Picha: AP


Waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier ameitaka China kuendeleza zaidi mazungumzo na wajumbe wa kiongozi wa kidini wa Tibet anayeishi uhamishoni Dalai Lama. Steinmeier ameyasema hayo wakati wa ziara yake nchini China ambapo viongozi wa nchi hiyo wamesema uhusiano kati ya nchi hizo mbili unarejea katika hali bora baada ya mvutano kuhusiana na suala la Dalai Lama.




Kufuatia mazungumzo mjini Beijing leo Ijumaa, Frank-Walter Steinmeier na mwenzake wa China Yang Jiechi pia amesema wamekubaliana kuanzisha mikutano ya mara kwa mara kuhusiana na masuala ambayo ni pamoja na mabadiliko ya hali ya hewa na haki za binadamu katika ishara za kuimarika kwa uhusiano baina ya nchi hizo mbili.


Uhusiano baina ya China na Ujerumani umekuwa kwa taratibu ukirejea katika hali ya kawaida tangu pale kansela wa Ujerumani Angela Merkel alipomwalika Dalai Lama katika makao makuu ya kansela mjini Berlin mwaka jana.

Akizungumza na waandishi wa habari, waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier amesema wamejadili hali katika jimbo la Tibet , jimbo ambalo waandishi wa habari wa kigeni wamezuiwa kuingia pamoja na watalii kutoka nje tangu pale ghasia dhidi ya serikali zilipozuka miongoni mwa Watibet katikati ya mwezi wa March.


Ghasia hazimsaidii yeyote. Kile tunachokitaka , ni uwazi kuhusiana na utaratibu wa Tibet binafsi.

Na tunahitaji njia ya kuelekea katika majadiliano pamoja na wawakilishi wa Tibet. Njia ambayo China binafsi inapaswa kuifuata. Tunalazimika kuitolea wito zaidi China, kuweza kujizuwia pamoja na kutoa uamuzi sahihi, yanapotokea maandamano ama matukio mengine ya kila siku.


Waziri wa mambo ya kigeni wa China Yang amesema kuwa uhusiano kati ya China na Ujerumani tayari umeingia katika hatua za kawaida za maendeleo, na kuiita ziara ya Steinmeier kuwa tukio kubwa katika uhusiano baina ya nchi hizo mbili.

China inaamini kuwa Dalai Lama anajaribu kulipatia jimbo la Tibet uhuru licha ya matamshi ya mara kwa mara kuwa si hivyo, na mara kwa mara inawashutumu wanasiasa kutoka mataifa mengine wakikutana nae.

Steinmeier ambaye baadaye leo Ijumaa alikutana na waziri mkuu wa China Wen Jiabao, anapendelea diplomasia ya kimya kimya kuhusiana na Tibet, suala ambalo limekuwa nyeti sana kutokana na ukandamizaji wa China dhidi ya ghasia katika mji mkuu wa jimbo la Tibet wa Lhasa March 14.

Ghasia hizo zilizuka baada ya siku nne za maandamano ya amani dhidi ya utawala wa miaka 57 wa China. Viongozi wa Tibet wanaoishi uhamishoni wanasema kuwa zaidi ya Watibet 200 wamekufa katika ukandamizaji huo. China inakana madai hayo na kusema watu waliofanya ghasia katika jimbo la Tibet wanahusika na vifo vya watu 21.


Uhusiano mzuri na wa karibu , baina ya Ujerumani na China unapatikana katika utamaduni wa muda mrefu, lakini pamoja na hayo, hatuwezi kuficha , kwamba wiki pamoja na miezi iliyopita haikuwa mizuri kwa uhusiano kati ya nchi hizi mbili. Kutokana na hilo nafurahi kusema kwamba, kukutana kwetu leo ni ishara, kwamba sasa uhusiano wetu unarejea.


Wen amemwambia Steinmeier leo kuwa maslahi yao ya pamoja baina ya China na Ujerumani ni makubwa kuliko tofauti zilizopo. Steinmeier amejiweka mbali na mkutano wa Merkel na Dalai Lama wakati kiongozi huyo wa kidini alipozuru Ujerumani mwezi uliopita.

►◄