1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri wa Mambo ya Nje wa Libya, Mussa Kussa amejiuzulu.

31 Machi 2011

Waziri wa Mambo ya Nje wa Libya,Mussa Kussa amekimbilia uhamishoni nchini Uingereza na kutangaza kwamba amejiuzulu wadhifa huo.

https://p.dw.com/p/10lIA

Mapambano yanaendelea nchini Libya, huku Kujiuzulu kwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Libya, Mussa Kussa kukielezwa kuwa siku za utawala wa Muammar Gadhafi zinahesabiwa. Mussa Kussa hivi sasa yupo Uingereza wakati huu vikosi vya Gadhafi vikiongoza mashambulizi ya ardhini dhidi ya Waasi.

Akizungumza na kituo cha televisheni cha France 24, Waziri wa zamani wa Uhamiaji wa Libya ambae kwa hivi sasa anaeishi uhamishoni, Ali Errishi amesema hatua hiyo inaashira sasa watu wengine watapata fursa ya kuingoza nchi hiyo.

Libyen Außenminister Moussa Koussa Kussa
Waziri wa Mambo ya Nje ya Libya, Mussa KussaPicha: AP

Waziri huyo alisisitiza kwamba mara nyingi amekuwa akieleza kwamba, yeye na kiongozi huyo waliwekwa kizuizini mjini Tripoli na inashangaza kuona amewezaje kutoroka nchini humo.

Aidha amesema kuondoka kwa Mussa Kussa kuna maana kwamba Gadhafi kwa hivi sasa hana mtu wa kuaminika zaidi ya yeke na watoto wake.

Waziri huyo wa zamani, Ali Errishi aliondoka mapema Februari nchini Libya baada ya kuanza vuguvugu la kutaka kumuondoa madarakani Kanali Gadhafi.

Ofisi ya Mambo ya Nje ya Uingereza imethibitisha uwepo wa Mussa Kussa nchini humo kwa kusema ameingia kwa ridhaa yake akitokea nchini Tunisia.

Kiongozi huyo anatajwa kuwa ni nguzo muhimu katika serikali ya Gadhafi kwa kuwa ndiye alikuwa akishughulikia masuala muhimu ya kidemokrasia kabla ya kuanza kwa machafuko.

Mussa Kussa mwenye umri wa miaka 59, amekuwa Waziri wa Mambo ya nje tangu mwaka 2009, baada ya kuwa mkuu wa usalama wa taifa wa nchi hiyo tangu 1994.

Wakati hayo yakitokea, jumuiya ya Kujihami ya NATO leo imechukua mamlaka yote ya kutekeleza operesheni ya kuzuia ndege kuruka nchini Libya iliyoidhinishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa Machi 19 mwaka huu.

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa NATO, Anders Fogh Rasmussen, jumuiya hiyo inayojumuisha nchi 28, itaratibu operesheni yote ya anga nchini humo.

NO FLASH Libyen Krieg Gaddafi Brega Rebellen NATO
Waasi wakiwa katika mapambano nchini LibyaPicha: picture alliance/dpa

Mapambano yanaendelea katika maeneo tofauti nchini Libya. Gadhafi anatajawa kuyadhibiti karibu maeneo yote yaliyochukuliwa na waasi wiki iliyopita yakiwemo, Ras Lanuf, Uqayla na Brega huku waasi wakiwa wametawanyika tawanyika katika maeneo tofauti.

Vyombo vya habari vimesema Gaddafi amekuwa akiwatawanya kwa kutumia vifaru pamoja na mizinga ya masafa marefu.

Mmoja kati ya mpiganaji muasi ambae hakuweza kufahamika jina lake alisema "Tulikuwa Ras Lanuf,Vikosi vya Gadhafi vikatushambulia kwa mabomu, kwa hiyo tukalazimika kurejea nyuma ya Ras Lanuf".

Hata hivyo waasi hao waliopoteza nguvu wakati wote wamekuwa wakihimiza vikosi vya anga vya Muungano vifanye mashambulizi dhidi ya vikosi vya Gadhafi ili waweze kurejea katika maeneo walikofurushwa na hatimae kushika hatamu ya uongozi wa Libya.

Mwandishi-Sudi Mnette/AFP/RTR

Mhariri/Josephat Charo