1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri wa mazingira wa Ujerumani Röttgen atimuliwa

Abdu Said Mtullya17 Mei 2012

Kansela Angela Merkel amemwachisha kazi Waziri wake wa mazingira Nobert Röttgen siku chake baada ya Waziri huyo kushindwa katika uchaguzi wa Bunge katika jimbo la Northrhine Westphalia.

https://p.dw.com/p/14wy9
Waziri wa Mazingira Norbert RöttgenPicha: dapd

Hadi jumatatu iliyopita , siku moja baada ya kufanyika uchaguzi wa jimbo la NorthrhineWestphalia Kansela Merkel alitangaza kwamba Röttgen angeliendelea kuwa Waziri wa mazingira wa Ujerumani

Lakini kutokana na kushindwa katika uchaguzi wa Bunge katika jimbo hilo Waziri Röttgen mwenyewe alitangaza kujiuzulu uenyekiti wa chama chake cha CDU katika jimbo la Northrhine Westphalia.

Röttgen alikuwa mgombea Uwaziri Mkuu kwa niaba ya chama chake cha CDU jumapili iliyopita lakini aliaungushwa vibaya, kwa kupata asilimia 26,3 ya kura.

Hayo ni matokeo mabaya kabisa katika historia ya chama cha CDU katika jimbo la Northrhine Westphalia lenye watu milioni 18 linaloongoza kwa idadi ya watu nchini Ujerumani.

Kansela Merkel amemshukuru Nobert Röttgen kwa mchango wake na hasa kazi aliyoifanya katika ulinzi wa mazingira

Kansela Merkel amemteua kiongozi wa wabunge wa vyama vya CDU na CSU Peter Altmaier kuchukua nafasi ya Nobert Röttgen.

Angela Merkel na Norbert Roettgen
Angela Merkel na Norbert RoettgenPicha: dapd

Makamu wa Kansela,Philipp Rösler ambaye pia ni Waziri wa uchumi wa Ujerumani amesema kuteuliwa kwa Peter Altmaier kunaonyesha dhamira ya kudumisha ushirikiano imara katika serikali ya mseto.

Vyama vya upinzani vimeitathmini hatua ya kuachishwa kazi kwa Waziri wa mazingira kuwa ni dalili ya kushindwa kwa Kansela Merkel.

Mwenyekiti wa chama cha kijani Cem Özdemir amesema kuwa Röttgen ametolewa mhanga.Mwenyekiti huyo ameeleza kuwa hatua ya Kansela Merkel ni kujaribu kufunikiza kushindwa katika uchaguzi wa jimbo la Northrhine Westphalia na pia ni kujaribu kupoteza lengo la mageuzi ya nishati. Özdemir amesema kuzibadilisha sura tu hakutasaidia.

Katibu Mkuu wa chama kikuu cha upinzani cha SPD Andreas Nahles amesema kutimuliwa kwa Waziri wa mazingira Nobert Röttgen ni ushahidi mwingine wa kuonyesha hali mbaya katika serikali ya Kansela Merkel.

Mwandishi:Marcel Fürstenau
Tafsiri:Mtullya Abdu.
Mhariri: Josephat Charo