1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri wa Nje wa Ujerumani ziarani Mashariki ya Kati

2 Juni 2008

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani,Frank-Walter Steinmeier akiendelea na ziara yake ya Mashariki ya Kati, amekutana na wajumbe wa serikali ya Israel mjini Tel Aviv.

https://p.dw.com/p/EBCL
Waziri wa Nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier (kulia) na Rais wa Lebanon Michel Suleiman walipokutana Baabda kwenye Ikulu ya rais karibu na Beirut,Jumapili Juni 1,2008.Picha: AP

Kwa sababu ya mzozo wa ndani wa kisiasa unaokutikana Israel hivi sasa,Steinmeier hajakutana na Waziri Mkuu Ehud Olmert anaekabiliwa na shutuma za rushwa.Badala yake,amekutana na Waziri wa Ulinzi Ehud Barak na Waziri wa Nje Zipi Livni mjini Tel Aviv.Majadiliano hayo yamehusika na mkutano wa usalama wa maeneo ya Kipalestina unaotazamiwa kufanywa Juni 24 katika mji mkuu Berlin nchini Ujerumani.Lengo la mkutano huo ni kujadili mipango ya kuimarisha mifumo ya usalama na sheria katika taifa la Palestina litakaloundwa.

Mada inayopewa kipaumbele na Steinmeier katika mazungumzo yake ni mchakato wa amani wa Mashariki ya Kati uliokwama.Kwani Waisrael na Wapalestina kwenye mkutano wa Annapolis Novemba 2007 uliozinduliwa na Rais wa Marekani George W.Bush kufufua majadiliano ya Mashariki ya Kati,pande hizo mbili zilikubaliana kukamilisha mswada wa mkataba,juu ya kuwepo kwa mataifa mawili.

Steinmeier leo anakutana vile vile na Rais wa Wapalestina Mahmoud Abbas mjini Ramallah.Baadae ataelekea Jenin,kaskazini mwa Ukingo wa Magharibi ambako ataeleza mradi unaotazamia kujenga uwanja utakaokuwa na viwanda kadhaa,ikitazamiwa kuwa nafasi mpya za ajira zitapatikana kwa maelfu ya Wapalestina.

Waziri Steinmeir aliianza ziara yake ya Mashariki ya Kati nchini Lebanon ambako siku ya Jumapili alikutana na Rais Michel Suleiman aliechaguliwa hivi karibuni.Steinmeier ni Waziri wa Nje wa kwanza kutoka Umoja wa Ulaya kukutana na rais mpya wa Lebanon aliechaguliwa kufuatia makubaliano ya Doha ya Mei 21 yaliyomaliza mgogoro wa kisiasa nchini humo.Steinmeier amesema,Libanon itasaidiwa katika juhudi zake za kuijenga upya nchi hiyo.Akaongezea:

"Kama iwezekanavyo nchi za Ulaya ikiwa ni pamoja na Ujerumani,zinataka kusaidia utaratibu huo,kwani kuondoshwa vikwazo mjini Beirut,kuchaguliwa kwa rais mpya pamoja na serikali mpya inayotazamiwa kuundwa katika siku au majuma machache yajayo - hayo yote ni ishara ya matumaini kwa umma wa Lebanon."

Steinmeier vile vile alitembelea kikosi cha wanamaji wa Ujerumani,walio sehemu ya UNIFIL-tume ya Umoja wa Mataifa inayosaidia kulinda amani Lebanon.Manowari ya Ujerumani inasaidia kulinda pwani ya Lebanon ili kuzuia usafirishaji haramu wa silaha katika eneo hilo.